Header Ads

ad

Breaking News

RAIS SAMIA AWATAKA VIONGOZI KUWEKA KUMBUKUMBU ZA HISTORIA ZAO

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

 RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuwa na utamaduni wa kuweka kumbukumbu zao kwa ajili ya maslahi yao na taifa, huku akitoa rai kuanzishwa kwa tovuti ya serikali itakayoweka kumBukumbu za viongozi.

Hayo ameyasema leo Septemba 30,2023, wakati akizindua tovuti ya kuhifadhi nyaraka za Dkt.Salim Ahmed Salim, hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius nyerere (JNICC).

Amesema familia ya Dkt.Salim ndiyo waliokuja na wazo hilo la kuweka tovuti maalumu hivyo, ni wakati sasa wa serikali kufikiria namna ya kuanzisha tovuti ya serikali kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za viongozi.

“Hili ni wazo la familia ambalo lililetwa kwetu, kama serikali nikaona ni jambo Zuri na nikaelekeza serikali kulisimamia, lakini hili kwetu limetuamsha na kutukumbusha umuhimu wa kuhifadhi historia zetu,” amesema Dkt.Samia.

Rais amesema kuwa, tovuti hiyo itaakisi safari ya maisha halisi ya Dkt.Salim Ahmed Salim, pia itatoa fursa ya kutambua historia ya nchi.

Amesema Dkt.Salim alifanya makubwa Afrika na duniani kote, ikiwemo kuanzisha baraza la usuluhishi na kuwa katibu mkuu wa kwanza kwenda Afrika Kusini kupambana na ubaguzi wa rangi. 

“Hizi ni hazina kwa taifa, viongozi waliopo na watakaokuja wanapaswa kujifunza ikiwemo uvumilivu kama alivyo Dkt.Salim,” amesema.

Ameitaka taasisi ya uongozi kumsaidia Rais wa awamu ya nne kukamilisha kitabu chake na kukiweka kwenye tovuti.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema chuo cha Diplomasia kwa sasa ni mali ya serikali na amekibadilisha jina na kukiita Kituo cha Diplomasia cha Dkt.Salim Ahmed Salim.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati akimkaribisha Rais, amesema hiyo ni tovuti ya kwanza kwa kuhifadhi nyaraka za serikali.

Amesema wizara itaongeza bajeti kwa mwaka huu wa fedha ili kuongeza nguvu kwenye kuhifadhi wa kumbukumbu, ikiwezekana kufungua tovuti ya serikali ambayo itatumika kuweka kumbukumbu za viongozi.

"Taasisi ya Uongozi ndiyo iliyosimamia upatikaji wa hii tovuti, pia walisimamia kitabu cha Rais wa awamu ya pili Dkt.Ally Hassan Mwinyi na kitabu cha Rais wa awamu ya tatu hayati Dkt Benjamin Mkapa."

"Nafikiri huu ni wakati sahihi wa kuanza kuweka kumbukumbu za viongozi wakiwa hai ili historia zao ziweze kuwa funzo kwa vijana ambao ndiyo viongozi wa kesho,” amesema Simbachawene.

Naye,Balozi Christopher Lihundi, amewataka vijana kutumia tovuti hiyo kama sehemu ya urithi wa Bara la Afrika ili kujifunza mambo mbalimbali, yakiwemo ya uongozi.

Balozi Lihundi amewataka wanasiasa kuiga uvumilivu kama aliokuwa nao Dkt.Salim Ahmed Salim.

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema mawazo ya Dkt.Salim yalizingatia zaidi utaifa hivyo, ni wakati wa viongozi kujifunza kupitia maandiko yake mbalimbali yaliyoko kwenye tovuti.

Mtoto wa Dkt.Salim, Ahmed Salim ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika jitihada zao za kuandaa tovuti hiyo ambayo itatoa elimu ya namna ambayo aliishi Dkt.Salim katika maisha ya uongozi.

Amesema tovuti hiyo itakuwa endelevu na itapatikana bila gharama, lengo likiwa kila mtu kujifunza na kuijua historia ya nchi.

Dkt.Salim Ahmed Salim alikuwa waziri mkuu wa tano na Katibu Mkuu wa nane, lakini pia alikuwa mwanadiplomasia mwenye mchango mkubwa kwa taifa.

Sasa hivi ni mgonjwa, ambapo leo ameshindwa kuhudhuria tukio hilo muhimu kwenye maisha yake na kuwakilishwa na familia yake.

No comments