Header Ads

ad

Breaking News

LATRA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE, WAMSHUKURU RAIS SAMIA


Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA. Habib Suluo akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Alhamisi Oktoba 19, 2023, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), imesema imeongeza mapato kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa kukusanya shilingi bilioni 34.17 ikiwa ni nyongeza ya shilingi bilioni tano sawa na asilimia 20, ikilinganishwa na mwaka 2021/22, ambao walikusanya shilingi bilioni 28.53.

LATRA imepata mafanikio hayo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa mwongozo wa ufuatiliaji wa mapato kwa mamlaka hiyo, kwani mwaka 2020/ 21 ilikusanya shilingi bilioni 25.945 na mwaka 2021/22 mapato yaliongezeka kwa kukusanya shilingi bilioni 28.53, sawa na ongezeko la asilimia 10.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo, ametoa taarifa hiyo Alhamisi Oktoba 19,2023 jijini Dar es Salaam,m wakati wa kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini na kufafanua kuwa, mapato hayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka jambo ambalo wataendelea kujivunia.

“Mapato yanapoongezeka huwa tunachangia mfuko wa Serikali na hii ni mafanikio makubwa sana kwetu, kuna taasisi ili zijiendeshe zinapewa fedha na Serikali kwa, upande wetu ni tofauti ingawa sheria inatutaka katika nyongeza ya mapato yetu turejeshe asilimia 15,” amesema.

Ameongeza kuwa, katika asilimia 15 ya faida ambayo wanatakiwa kurejesha serikalini baada ya kupata faida, kwa mwaka 2020/21 walipeleka katika mfuko wa Serikali shilingi bilioni 3.5 na  mwaka 2021/22 walipeleka shilingi bilioni 4.2, huku mwaka 2022/23 wamefanikiwa kupeleka shilingi bilioni 4.7. 

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya mamlaka yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 25.95 hadi shilingi bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG), ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 8.22, sawa na ongezeko la asilimia 32.

“Mapato yatokanayo na adhabu yamepungua na mapato yatokanayo na leseni kujenga tabia ya utii wa Sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini,”amesema.

CPA Habibu Suluo amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha LATRA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi na hivyo, imeipa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mkurugenzi Mkuu huyo anesema kuwa, kutokana na kutekeleza majukumu yao vizuri, tangu LATRA ianze shughuli zake hawajapata hati chafu na siku zote hupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwao ni jambo la kujivunia na kujipongeza.

“Tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo yake kwetu katika kufuatilia makusanyo na kujipanga vema katika shughuli zetu, na kutokana na umahiri wa uongozi wake ndiyo sababu tumefikia mafanikio haya,” amesema.

CPA Suluo amesema katika usafiri wa barabara, kwa kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka leseni 230,253 hadi leseni 284,158, ikiwa ni sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1) ( b) cha Sheria ya LATRA, Mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, hivyo mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara. Leseni hizi hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. Leseni hizi hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa,” amesema.

Amesema kuwa, mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa kwa lengo la kupata madereva wenye sifa na weledi kuendesha magari yanayotoa huduma kwa usafiri wa umma, kwa kupima umahiri wao hasa maarifa waliyopata ili kuimarisha usalama.
 
“Hadi kufikia Septemba 30, 2023, madereva 17,990 wamesajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya mamlaka, ambapo madereva 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa wa LATRA. Miongoni mwa madereva hao, madereva wa mabasi 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button). Matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo wa VTS.”
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema mfumo wa kufuatilia mwendokasi wa mabasi ulioanza kutumika mwaka 2017, hadi sasa zaidi ya magari 9,420 yameunganishwa na mfumo huo, wakati magari 7,620 yapo hai na yanaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo huu. 

“Mfumo umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na mwendokasi, umepunguza madhara ya ajali zinazotokana na mwendokasi na umerahisisha uchunguzi wa ajali zinapotokea.”

Amesema kuwa, sheria inawataka kusajili wahudumu, hivyo wapo katika mchakato wa kuwapata kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Biashara kwa kuandaa mitaala ya kufanikisha hilo.

Kuhusu migogoro, CPA Suluo amesema kuwa ofisi yake imefanikiwa kumaliza migogoro 234 katika kati ya watoa huduma wenyewe kwa wenyewe na watoa huduma na abiria bila kufika ngazi za juu kwa ajili ya utatuzi.

Mkurugenzi Mkuu huyo ametoa wito kwa wanaoingia kwenye migogoro ikiwemo kwa abiria kupotelewa kwa mizigo yao au watoa huduma wenyewe kwa wenyewe wasiporidhiki na maamuzi wanatakiwa kukata rufaa Bodi ya Latra nasi kukimbilia kwa waziri au wakuu mikoa kwani huko si sehemu sahihi.

“Ushauri wangu ili kuondosha upotevu wa mizigo ni vizuri mzigo ukaandikwa namba ya simu, namba ya siti ya abiria na jina, hii itasaidia kuondoa changamoto ya kupotea ingawa changamoto kubwa imejitoeza zaidi Kahama, jambo lililofanya tuweke ofis yetu pale,” amesema.   

Kaimu Mkurugenzi Usafiri wa Reli, Mhandisi Hanya Mbawala.

Afisa Uhusiano na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza jambo wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Alhamisi Oktoba 19, jijini Dar es Salaam.

 Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, Salum Pazzy, Afisa Uhusiano na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim S.Salim na Mhariri wa Habari Leo, Mgaya Kingoba, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Oktoba 19,2023 jijini Dar es Salaam. 





Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena (aliyesimama), akizungumza jambo kwenye kikao kazi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kilichofanyika Alhamisi Oktoba 19,2023 jijini Dar es Salaam.



              Wahariri na waandishi wa habari wakiwa makini katika kikao kazi

No comments