Header Ads

ad

Breaking News

LATRA KUTOA MWONGOZO USAFIRI WA WAYA

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo akielezea mafanikio ya mamlaka hayo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jijini Dar es Salaam, Oktoba 19,2023.

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo, amesema  mamlaka hiyo ipo mbioni kutoa mwongozo kwa waendeshaji wa usafiri wa waya ambao wanatarajia uwekezaji huo utafanyika zaidi katika sekta ya utalii.

“Usafiri wa waya wenzetu wanautumia kwa ajili ya utalii, starehe na kuwahi maeneo ambayo yanaonekana kuwa na foleni.

“ssi tunachotoka kufanya ni kuangalia ni namna gani ambavyo usafiri huu utakuwa na tija hapa nchini hususan, sekta ya utalii.

“Lengo ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya utalii nchini, LATRA hatuwekezi huko bali, tunaweka miongozo, kanuni za udhibti wa usafiri huo.”

CPA Suluo ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2023 katika kikao kazi baina ya LATRA na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkurugenzi Mkuu amesema wadau wa LATRA ni wasafirishaji wa mabasi ya njia ndefu na mabasi ya miji na majiji, magari ya mizigo, madereva wa mabasi na malori, wakiwemo watoa huduma wa magari maalum ya kukodi, teksi mtandao, abiria, taasisi za umma na wananchi.

Leo LATRA, ni taasisi ya 20 ambayo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni kutekeleza maono ya Msajili Nehemiah Mchechu, anayesisitiza kuwa, suala la utawala bora katika mashirika hayo ni jambo ambalo halikwepeki, kwani lazima kila aliyeaminiwa awajibike ili mashirika hayo yaweze kuleta matokeo chanya.

Kupitia vikao kazi hivyo, wanapata nafasi ya kuelezea wanafanya mambo gani, wanaelekea wapi na yapi matarajio ya mashirika hayo na kwamba, mikutano hiyo ni muhimu kwa wahariri ambao kupitia vyombo vyao watafikisha taarifa sahihi kwa umma.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika ya umma, ndani ya hayo mashirika ya umma wana mashirika yenyewe, taasisi na kampuni ambapo zipo zaidi ya 298, miongoni mwa hizo kuna taasisi ambazo zinatoa huduma na zinafanya biashara huku nyingine zikijiendesha kibiashara, aidha kati ya hizo Serikali inamiliki hisa chache ambazo ni chini ya hisa asilimia 50.

Lengo la Serikali ni kuona mashirika hayo yanafikia lengo lake, ikizingatiwa kwamba yameanzishwa kwa mujibu wa sheria, mashirika haya kwa kiasi kikubwa yamefikia kiwango cha kuridhisha japo kuna machache ambayo hayajafikia malengo.

Mbali na hayo, CPA Suluo amesema, LATRA ni mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.

Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). “LATRA imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususani usafiri wa mizigo na abiria.”

Usafiri ambao unajumuisha mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Amesema malalamiko makubwa ambayo wanayapata mijini ni pamoja na daladala kukatisha ruti. Kutokana na changamoto hiyo, amesema wameweka namba maalumu ambazo abiria wakiona daladala inakatisha ruti au kufaulisha wawasiliane nao ili waweze kuchukua hatua za haraka.

Mkurugenzi Mkuu huyio amesema LATRA inawezesha matumizi ya teknolojia kama suluhisho kwa changamoto katika sekta ya usafiri.

Amesema, hayo yanafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi. CPA Habibu Suluo amesema, moja ya mafanikio yanayotambuliwa ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

Mfumo huu umekuwa ukifanya kazi tangu mwaka 2017 na umeonesha matokeo chanya katika kuokoa maisha na mali.

“LATRA itaendelea kutumia teknolojia kutatua changamoto za usafiri nchini.” Pia, amesema, kazi za mamlaka zimeainishwa katika kifungu cha tano cha Sheria Na.3 ya LATRA ya mwaka 2019 ikiwemo kutekeleza majukumu ya Sheria za Kisekta.

Amesema, wanatoa leseni, kuhuisha leseni na kufuta leseni pale ambapo wanabaini mtoa huduma anahatarisha usalama wa wananchi.

“Lakini, hatujawahi kufuta leseni moja kwa moja.” Katika hatua nyingine, CPA Habibu Suluo amesema kuwa, “Sisi LATRA kazi yetu tunaona inaenda vizuri sana kutokana na uongozi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Kwa namna ya kipekee tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweka muundo mzuri wa uongozi ambao unatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.”

Amesema mchango wa sekta binafsi katika Sekta ya Usafrishaji hapa nchini ni mkubwa, hivyo wataendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Majukumu mengine, CPA Habibu Suluo amesema ni kutoa, kuhuisha, au kufuta leseni za usafirishaji na kwamba, kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kisekta, LATRA inawajibika kusimamia viwango vya ubora wa huduma na usalama katika sekta zinazodhibitiwa.

CPA Habibu Suluo amesema wanaratibu shughuli za usalama wa usafiri ardhini, kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini.

Jukumu lingine ni kuhakikisha na kuthibitisha hali ya usalama wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini kwa matumizi.

“Kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia viwango vya uwekezaji, gharama, upatikanaji na ufanisi wa huduma.”

CPA Habibu Suluo amesema wanashughulikia na kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko na kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa mamlaka.

“LATRA tunahudumia na kuwajali wadau wetu wote wanaotumia usafiri wa barabara pamoja na usafiri wa reli."

Wahariri wa habari wakifuatilia maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo (hayupo pichani)

Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini, Fahamueli Mkeni.

Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA, Johansen Kahatano akizungumza katika kikao kazi hicho

Kaimu MKuu wa Kitengo cha  Uhusiano na Mawasiliano LATRA, Salum Pazzy, akifafanua jambo katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari

Afisa Uhusiano na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akifafanua jambo katika kikao kazi hicho

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo (katikati), Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara (kushoto) na  Kaimu MKurugenzi Udhibiti Uchumi, Fahamueli Mkeni, wakiandika maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wahariri katika kikao kazi hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo (katikati), akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania, Salim S.Salim (kulia) na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Ofisa ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, baada ya kikao kazi kilichofanyika leo Oktoba 19,2023 



No comments