CCM Vigwaza yapiga hodi Lions Club
Rais mstaafu wa Lions Club ya jijini Dar es Salaam, Muntazir Bharwan |
Na Omary Mngindo, Ruvu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Bagamoyo Pwani, imepiga hodi kwa uongozi wa Lions Club ya jijijini Dar es Salaam kuhusu kuboresha jengo lao ili liwe la kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa chama hicho, Athuman Kimui aliwasilisha ombi hilo kwa Muntazir Bharwan aliyeambatana na viongozi wa klabu hiyo katika hafla fupi ya kupokea vitabu na madaftari, vitakavyopelekwa katika shule za msingi katani hapa.
Alianza kwa kuupongeza uongozi huo kwa kusema kuwa, umekuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli za kimaendeleo katika kata hiyo, huku akigusia msaada wa vifaa tiba vilivyopokelewa katika Zahanati ya Ruvu Darajani miezi michache iliyopita.
"Lions mara kadhaa mnatupatia zawadi mbalimbali tunawashukuru sana, kipindi hiki tunakwenda kwenye chaguzi ofisi yetu haioneshi kama ya Kata, ipo pale Vigwaza Kambini na ndiyo iliyomtambulisha Diwani wetu Mohsin Bharwan, ile ofisi imechoka, tupo njiani kukuletea barua uone namna ya kutusaidia," alisema Kimui.
Akizungumzia ombi hilo, Bharwan aliwataka viongozi hao kuwasilisha barua yao inayohusiana na ombi hilo, ili uongozi huo ukaone ni namna gani unavyoweza kuunga mkono katika maboresho ya ofisi hiyo.
"Ombi lenu limesikika, viongozi wa Lions Club mbele yenu wapo wanachama wenzangu Hussam Dawoodbhai, Gulam Dossaj, Mohamed Mulla, Firoz Bandali na Nimira Gangji, leteni barua tuone ni namna gani tutavyoweza kuona uwezekano wa kusaidia," alisema Bharwan.
Naye Gama alisema kuwa, wanatambua mchango mkubwa unaondelea kutolewa na klabu hiyo, huku akiwaomba wana Vigwaza kuwaombea dua viongozi hao waendelee kusaidia katika nyanja mbalimbali, huku naye akichomekea changamoto ya matenki, ambapo Bharwani ameahidi kuanza na mawili kabla ya mwaka kumalizika.
Lions Club imekabidhi vitabu na madaftari kwa shule za msingi 15 vyenye thamani ya shilingi 802,000 vinavyolenga kuboresha ufundishaji na usomaji kwa walimu na wanafunzi.
Diwani wa Kata ya Vigwaza, Mussa Gama |
No comments