Bodi ya Mikopo yanufaisha wanafunzi 754,000
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul -Razaq Badru akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika leo Oktoba 26, 2023 jijini Dar es Salaam.
Na Frank Balile
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), imewanufaisha watanzania zaidi ya 754,000 ambao wamesoma kupitia mikopo tangu ilipoanzishwa mwaka 2004.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 26,2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, amesema kuanzia mwaka 1994/95 hadi hivi sasa, uwekezaji wa shilingi trilioni 7.2 umewanufaika wanafunzi 754,000.
"Bodi imewekeza shilingi trilioni 7.2, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1994/95 hadi sasa, ambazo zimewanufaisha wanafunzi 754,000, haya ni mafanikio makubwa,"amesema.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa, Bodi imefanikiwa kukusanya shilingi trillion 1.34, kati ya shilingi trilioni 2.1, kutoka kwa wanufaika wa mikopo. sawa na asilimia 64.
Katika kikao kazi hicho kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Msajili Nehemia Mchechu, imeelezwa kwamba, hadi sasa utekelezaji wa marejesho ya mikopo ya wanufaika bado kuna kiasi cha shilingi bilioni 758, ambacho wanufaika hawajarejesha.
Badru amesema kuwa, wanaendelea kuwafuatilia wanufaika wa mikopo hiyo ambao ni Wanafunzi wa elimu ya juu ili waweze kulipa na kutumika kwa wahitaji wengine.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa, kwa upande wa utoaji mikopo, Bodi yake haina upendeleo wowote, wanafuata kanuni na taratibu zilizowekwa katika kuwapatia mikopo wanafunzi.
"Kwasasa tunawaomba watanzania walionufaika na mikopo, warejeshe ili fedha hizo ziwasaidie wengine, pamoja na hayo tunawaomba watanzania kutoa ushirikiano ili kuwapata wanufaika waanze kurejesha fedha hizo,"amesema.
Amesema kwa upande wa wanufaika kutoka sekta isiyo rasmi, wengi wameshindwa kujitokeza kwa hiari kurejesha mikopo waliyochukuwa, huku baadhi ya waajiri wakishindwa kuwasilisha makato sahihi na kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa, wanakamilisha ushirikiano wa kimkakati na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa HIfadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na wakala wa Biashara na Leseni (BRELA).
Ameongeza kuwa, mbali na taasisi hizo, pia atawashirikisha viongozi wa serikali za Mtaa na vijiji ili kuwabaini wanufaika.
Amesema wataanzisha kampeni ya #Fichua ili wananchi watoe taarifa za wanufaika wasiojitokeza kwa hiari na kuendelea kuboresha huduma za urejeshaji mikopo kidigitali ili kurahisisha wanufaika kulipa popote na kiasi chochote kwa urahisi.
Badru amesema kwa mwaka 2023/24, jumla ya wanufaika 229,652, wapo wa shahada, ufadhili wa Samia na Diploma, ambao ni namba kubwa ya wanufaika wa fedha zilizopo.
Ameongeza kwamba, kwa sasa huduma zao zote zinapatikana kupitia mifumo ya TEHAMA (online), huku akiwataka wateja kutumia mfumo huo kupata huduma na kwamba, mifumo yao imeunganishwa na GovESB (e-GA).
"Tunahimiza kuunganisha mifumo ili kuongeza ufanisi, teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), imeendelea kuwabeba katika utoaji huduma na taarifa kwa jamii," amesema.
Afisa Uhusiano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, amesema kuwa, ofisi ya msajii wa Hazina inaendelea kusimamia maslahi ya serikali kwenye taasisi za umma, wakiamini kwamba, mali ya serikali ni mali ya umma.
Amesema taasisi na mashirika hayo wadau wake wakubwa ni umma, hivyo wanatarajia malengo ya kuanzishwa kwa taasisi na mashirika haya yaweze kutimia, kama wanatoa huduma iwe bora na kama biashara, pia iwe na faida kwa manufaa ya taifa.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia maono ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliona changamoto kwenye mashirika na taasisi yanafanya mambo mazuri, lakini hayafahamiki,” amesema Kosuri.
Amesema kuwa, ni fursa kwa taasisi za umma kupitia mikutano ya wahariri wa vyombo vya habari kuelezea malengo, mafanikio na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
No comments