Header Ads

ad

Breaking News

Serikali yaombwa kujenga maabara shule za msingi

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Chalinze Islamic, wakimfanyia upasuaji sungura


Na Omary Mngindo, Chalinze

SERIKALI imeombwa kuelekeza nguvu katika ujenzi wa maabara kuanzia elimu ya msingi kwa lengo la kuwapatia fursa wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo kuanzia ngazi hiyo.

Ushauri huo umetolewa na wanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Chalinze Islamic Modern iliyopo Chalinze Mzee, Kata ya Bwilingu katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, baada ya wanafunzi hao kumfanyia upauji sungura.

Wanafunzi hao waliwaambia waandishi wa habari shuleni hapo baada ya tukio hilo kuwa, mbali ya masomo ya kawaida, wanapatiwa mafunzo ya sayansi kwa vitendo, huku wakisema tukio hilo ni kiumbe wa tatu kumfanyia upasuaji.

Wanafunzi Lattifa Bakari na Mussa Swed wa darasa la tano na sita shuleni hapo, walisema wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji viumbe hao ambao wote wamefanikiwa na kwamba wapo hai.

"Nimeamua kuwekea mkazo somo la sayansi, nalipenda sana, matarajio yangu niwe daktari hapo baadaye, nawaomba wazazi waendeleze ndoto za watoto wao," alisema Lattifa.

Naye Swed alisema, "Nawashukuru walimu wetu wanatufundisha vizuri masomo mbalimbali likiwemo somo la sayansi,  tumemfanyia upasuaji sungura kama mlivyoshuhudia na yuko hai," alisema Swed.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Seif Hashimu, alisema shule yao imeamua kuwapatia masomo ya sayansi wanafunzi wao kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wakienda sekondari wasiwe wageni na masomo ya sayansi.

 Naye Mwalimu Issa Machame alisema kuwa, wanafundisha masomo hayo kwa lengo la kuwapatia taaluma wanafunzi wanaoanzia elimu ya msingi, ili hata watakapoingia sekondari wakikutana na masomo hayo wasiyaone mageni.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Chalinze Islamic wakimwonesha sungura waliyemfanyia upasuaji

No comments