Header Ads

ad

Breaking News

Sekta ya Bima imekua-Dkt.Saqware

             Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware 

Na Frank Balile

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware amesema sekta ya Bima nchini imekua kwa wastani wa asilimia 12.8, kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya Bima yameongezeka.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Dkt.Saqwre amesema sekta hiyo imekua kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka, ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka shilingi bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka 2021.

                      Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile

Dkt.Saqware amesema kuwa, mchango wa sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021.

"Mamlaka imeendelea kuongeza gawio serikalini,kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023, mamlaka imelipa gawio kwa serikali la jumla ya sh.bilioni 2.9, pia sekta hii imechangia kutoa ajira kwa vijana, ambapo hadi Septemba 2022, ajira za kudumu kwa watanzania 4,173.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amempongeza Kamishina wa TIRA kwa kazi nzuri wanayoifanya, huku akiwataka wazidi kushirikiana. 

Kamishna Dkt.Saqware amesema mamlaka imeendelea kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la ukatiaji wa bima za lazima, ukatiaji wa bima kwa mali za serikali na Bima ya Afya kwa wote.

Amesema kuwa, mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa  kushirikisha wadau wote kwenye sekta, lengo likiwa ni kufikia asilimia 80 ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18, ifikapo mwaka 2030.

"Tutaendelea na mpango wetu wa kutoa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta, malengo yetu ni kuwafikia asilimia 80 ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18," amesema Kamishna Dkt.Saqware.

Kamishna huyo amesema mamlaka inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kwa Wizara na Taasisi za Umma kutekeleza Sheria ya Bima Sura Na.394 YA 2009, na Sheria ya manunuzi Namba 7 ya mwaka 2011.

Amesema mkakati wa taasisi ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1) hadi (3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011, kif. 4 (2) (b).

"Hadi Julai 2023, mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo,Wizara ya Nishati, Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI.Mkakati huu ni endelevu na utazifikia Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Umma,"amesema Dkr.Saqware.







No comments