Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuimarika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Vyama vya Siasa na Msajili wa Vyama vya Siasa imesaidia kukuwa kwa masuala ya kisiasa yenye maslahi na Tanzania.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati akifunga Mkutano wa Baraza Maalum la Vyama vya Siasa uliokuwa ukitathmini utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi kazi na kujadili hali ya kisiasa Nchini uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar-es-salaam.
Amesema Mkutano huo wenye Kauli mbiu "Imarisha Demokrasia Tunza Amani" unakwenda kuimarisha Demokrasia Nchini kupitia Wadau wa Vyama vya Demokrasia ya Vyama vingi ambao wanashiriki katika kuliletea maendeleo Taifa la Tanzania.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Kikosi Kazi cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kimefanya kazi nzuri na ya aina yake ya kushughulikia masuala ya Demokrasia kwa kutoa maoni ya namna bora ya kuimarisha Demokrasia vya Vyama vingi sambamba na kudumisha Amani nchini.
Sambamba na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameeleza kuwa Serikali katika kuadhimisha azma ya kuimarisha Demokrasia nchini imezielekeza Taasisi za Serikali zilizotajwa katika Mapendekezo ya Kikosi kazi kufanya mazingatio ya utekelezaji wa maoni yaliyopendekezwa ambayo yataleta tija kubwa katika ukuaji wa Demokrasia nchini.
Aidha amefafanua kuwa watanzania wanaendelea na shughuli zao za kujipatia rizki kutokana na Amani na utulivu iliyopo ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kusimamia Amani isitoweke na kuendelea kuwaletea maendeleo watanzania bila ya kujali Itikadi zao za kisiasa.
Amewataka viongozi wa Vyama vya siasa kuwanasihi wanachama na mashabiki wa Vyama vya Siasa kulinda tunu ya amani iliyopo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu hasa wanapoendesha Mikutano ya Hadhara.
No comments