Header Ads

ad

Breaking News

MAVUNDE AITAKA TEITI KUWA KITOVU CHA TAARIFA ZA MADINI

 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde

Na Mwandishi wetu -Dodoma  

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameitaka Taasisi ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini (TEITI), kuwa kitovu cha taarifa za rasilimali madini ili kuisaidia serikali na wizara katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika rasilimali hizo ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa sekta ya madini nchini. 
Waziri Mavunde ametoa maelekezo hayo leo Septemba  wakati akizungumza katika kikao na TEITI pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC),  kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri Mavunde, amesema TEITI ina jukumu kubwa la kukusanya taarifa na takwimu zinazohusu rasilimali madini, ni matarajio kuwa taarifa au takwimu hizo zitaisaidia wizara katika mipango yake ya kuongeza mapato. 
“Sekta hii ni kubwa sana, ili kufikia lengo la kuongeza mapato ya serikali,  tunapaswa kuwa na taarifa sahihi zilizofanyiwa utafiti pamoja na takwimu sahihi za mapato ambazo zitaiongoza wizara kujua ni eneo gani linapaswa kuongezewa nguvu zaidi, hii ni kutokana na TEITI yenyewe kuwa ni kitovu cha taarifa zote zinazohusu rasilimali madini,” amesema.  
Akiizungumzia TGC, Waziri Mavunde amekitaka kituo hicho kusaidia Wizara kufikia lengo la kuongeza thamani madini ili kutimiza lengo la kuanzishwa kwake na kuyafanyia kazi yale mliyojifunza katika ziara ya China na Thailand. 
“Nimesikia mlitembelea China na Thailand, ni matumaini yangu mtayafanyia kazi yale mliyojifunza huko, ujuzi huo mlioupata huko, tunataka upatikane hapa nchini na tuwajengee uwezo watu wetu ili wafanye vizuri zaidi katika eneo hilo la kuongeza thamani madini yetu,” amesema Waziri Mavunde.  
Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa, amesema lengo la kuanzishwa kwa TEITI ni kuhakikisha wizara inakuwa na takwimu sahihi zinazohusu rasilimali madini ili zisaidie kufikia malengo yake, yakiwemo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. 


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TEITI, Mariam Mgaya, amesema TEITI imepanga kuweka wazi mikataba ya serikali na makampuni yaliyowekeza katika rasilimali zao ili kuweka uwazi wa mikataba hiyo. 

Amesema TEITI inatarajia kuweka wazi kiasi cha hisa za serikali kwa kampuni zinazoingia nayo ubia hapa nchini, ili wananchi wafahamu mawanda ya umiliki wa hisa ya serikali katika kampuni hizo na manufaa yanayopatikana. 
Amesema TEITI imepanga kufanya tafiti kwenye shughuli za sekta ya madini ili kuweka wazi kuhusu uharibifu wa mazingira sambamba na mchango wa wachimbaji wadogo katika sekta ya madini ambao kwa siku za karibuni umeongezeka sana. 
Akizungumza Kwa niaba ya Mratibu wa TGC, Kaimu Mratibu Msaidizi, Kurugenzi ya Mipango, Tafiti na Uendelezaji Ujuzi wa kituo hicho, Jumanne Shimba. amesema kituo hicho kimepanga kuwa na maabara yenye viwango vya kimataifa ili kutoa huduma za uongezaji thamani madini kwa viwango vya kisasa
Amesema kituo hicho kimepanga kuanzisha vituo vitakavyotangaza fursa ya madini nchini, kwani tayari wameaanza katika uwanja wa ndege cha wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), na mipango mingine ikiendelea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

No comments