Mafuru amshukuru Rais Samia kuifungua nchi , asema diplomasia ya mikutano yazidi kukua
Na Frank Balile
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC),Ephraim Mafuru, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua nchi kiuchumi.
Mafuru amesema kazi hiyo imechangia diplomasia ya mikutano nchini kuendelea kukua kwa kasi, jambo linalochangia kukuza pato la Taifa.
“Kwa sasa watu kutoka nje ya Tanzania wanaipenda wanaipenda nchi yetu, wanakuja kwa wingi, ninamshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuifungua nchi.
“Pamoja na Royal Tour, Rais Samia hushiriki mikutano mbalimbali kuitangaza nchi, hivyo Tanzania imeendelea kuwa chaguo muhimu na kuvutia mikutano mbalimbali ya Kimataifa.”
Akizungumza leo Septemba 14, 2023 katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, ikiwa ni mwendelezo wa vikao kazi baina ya taasisi na mashirika ya umma chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mafuru amesema, baada ya kampeni kubwa ya kufungua nchi, wamekuwa na asilimia 10 ya soko la hisa katika Afrika, hivyo wanandaa mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafikia malengo makubwa ya kuleta kwa wingi fedha za kigeni nchini.
“Arusha kama kitovu cha utalii, na sisi kama kitivo cha utalii, tunashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafanikisha shughuli hizo ili kuimarisha mnyororo wa thamani nchini,” amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Amesema wanashiriki kutangaza namna ambavyo wageni wanaweza kufika na fursa zilizopo wakijumuisha vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hasa jijini Arusha.
Mafuru amesema wanajisikia fahari kwa vituo vyao viwili ya AICC na JNICC, kuandaa mikutano mbalimbali ya Kimataifa, ambapo kumbe zao zina uwezo wa kutafsiri lugha tano.
Amesema, AICC na JNICC vimekuwa na uwezo mkubwa wa kuandaa mikutano mikubwa ya Kitaifa na kimataifa, huku akimshukuru Msajili wa Hazina, Nehemiah Msechu kwa kubuni jukwaa hilo ambalo linatoa fursa kwa taasisi na mashirika ya umma kuwaeleza watanzania wanachokifanya.
Amesema AICC ilianzishwa mwaka 1969 na kazi zao ni kuendesha mikutano wakiwa na kumbi za mikutano, nyumba za kupangisha na hospitali.
Amesema nguvu kubwa ni kuhakikisha diplopmasia ya mikutano inaendelea kuwa nguzo muhimu katika diplomasia ya uchumi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kupitia utafiti wao, wamebaini kuwa diplomasia ya mikutano ina mchango mkubwa katika kuongeza fedha za kigeni na kuimarisha uchumi nchini.
Kituo hicho hukodisha ofisi katika majengo yake ya makao makuu, makazi katika Manispaa ya Arusha na kuendesha hospitali.
Amesema mbali na AICC, pia wanamiliki na kuendesha Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) cha Dar es Salaam.
Amesema hospitali yao ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 90,000 kwa mwaka, pamoja na kutoa huduma ya afya, wamekuwa sehemu ya kutengeneza mapato.
Mafuru ameweka wazi kuwa, AICC na JINCC ni wanachama wa Taasisi ya AIPC (The International Association of Convention Centres), ambayo inaviunganisha vituo vyote vinavyotoa huduma za mikutano duniani.
“Ameongeza kuwa, wapokwenda kushiriki mikutano, wanajifunza, ambapo mwaka 2019 kabla ya UVIKO-19, Afrika iliandaa mikutano zaidi ya 450, lakini mwaka 2022 iliandaa mikutano zaidi ya 200, ambapo Tanzania iliandaa mikutano 15 kabla ya UVIKO-19, lakini baada ya 2022 ilianda mikutano 18, hatua ambayo ni kubwa.
Katika kila palipo mafanikio, Hapa kozi changamoto, Kwani hadi sasa wanazidai taasisi mbalimbali za serikali, zikiwemo binafsi zaidi ya shilingi bilioni 7.4
Ameweka wazi kuwa, taasisi na mashirika hayo yapo 20, kati ya hayo 17 ni ya Serikali, hivyo wanaziomba taasisi hizo zilipe madeni hayo ili vituo hivyo viweze kujiendesha kibiashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC, Ephraim Mafuru (katikati), akiwa na Mkurugenzi wa Mikutano na Masoko, Mkunde Senyagwa Mushi (kushoto), na Meneja wa Kituo cha Mikutano Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Catherine Kilinda, wakati walipokutana na wahariri wa vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam.
No comments