Header Ads

ad

Breaking News

MAAFISA HABARI, MAWASILIANO NA UHUSIANO ZANZIBAR WANOLEWA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Khatib Hassan, akifungua mafunzo ya siku mbili kwa maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano ya kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi. Kushoto ni Naibu Katibu Mtendaji Idara ya Mipango Tume ya Taifa ya UNESCO, Aboud Idd Khamis na mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa Zanzibar (SUZA), Imane Duwe Othman, katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MAAFISA wa Habari, Mawasiliano na Uhusiano nchini wametakiwa kuwa, wabunifu katika utendaji wa kazi zao ili kuendana na ukuwaji wa maendeleo ya teknolojia.

Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Khatib Hassan, ameyasema hayo  katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya waandishi na maafisa wa habari wa SMZ, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab.

Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza wigo mpana wa kupata taarifa nyingi na kwa haraka, kwani maafisa hao wanatakiwa kuwa wabunifu katika mawasiliano yao na umma ili maudhui yao yaweze kueleweka kwa urahisi na kuwavutia watu .

Amesema kuwa, maafisa wa habari wanapaswa kufahamu kwamba, wanaishi katika ulimwengu wa habari feki licha ya kwamba, kuna mabadiliko makubwa ya ukuwaji wa sayansi na teknolojia ya kupata habari kwa haraka.

Mkurugenzi huyo amesema maafisa hao wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha wanatoa habari sahihi na za kuaminika ili kuepusha upotoshwaji.

Hassan amewataka maafisa hao kuwa na mkakati maalum wa kukabiliana na changamoto na matukio yanayotarajiwa katika taasisi zao ili kutoa maelezo ya haraka wakati inapotokea hali ya taharuki katika taasisi hizo.

“Uadilifu na uaminifu katika kazi zenu ni jambo la lazima, mnapaswa kuwa waadilifu ili kujenga imani katika taasisi zenu na wadau wenu,” amesema.

Naibu Katibu Mtendaji Idara ya Mipango Tume ya Taifa ya UNESCO, Aboud Idd Khamis, amesema maafisa wa habari ni moja ya rasilimali muhimu katika taasisi hivyo , mafunzo hayo yatawasaidia kuwaongezea uwezo na maarifa katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Imane Duwe, amesema pamoja na mambo mengine, maafisa habari wana wajibu wa kushirikiana na watu, kujiamini na kujenga uthubutu.

Amesema wanapaswa kujua majukumu yao, kuwa wavumilivu na kuchakata data na kutoa taarifa za taasisi zao.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo ulinzi na usalama kwa waandishi na maafisa habari.  

Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wakisikiliza kwa makini mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Zanzibar.

No comments