BARABARA YA NEWALA-MASASI NI MUHIMU KWA USAFIRISHAJI WA MAZAO -RAIS SAMIA
![]() |
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akikata utepe |
Barabara hiyo inatajwa kupita maeneo ya kimkakati katika mtandao wa barabara ambako korosho hulimwa kwa wingi katika Wilaya za Tandahimba na Newala, hivyo itaunganisha wakulima na masoko kupitia Bandari ya Mtwara na Uwanja cha ndege wa Mtwara kwenda katika maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati akizinduzi barabara hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema, “Mara ya mwisho nilipopita kwenye kampeni wananchi mliomba kupata barabara, sasa tayari kilomita 50 zimeshakamilika na zilizobaki lazima tuzikamilishe hadi Masasi kwani barabara hii ni muhimu sana hasa kwa kusafirisha mazao kutoka mashambani kwenda sokoni.”
Rais Samia amewataka wananchi mkoani humo kudumisha amani, kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mazao kwa wingi ili Serikali ipate fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa faida ya watanzania
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema utekelezaji wa mkataba kwa sehemu ya Mtwara – Mnivata (km 50), umegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
“Hadi kukamilika kwa mradi huu, jumla ya shilingi 78,401,225,420.37 zimelipwa kwa mkandarasi, shilingi 4,614,877,406.77 zimelipwa kwa mhandisi mshauri na shilingi 70,435,260.94 zimelipa fidia ya mali na ardhi kwa wananchi walioathiriwa na mradi kwa mujibu wa sheria,” amesema Mhandisi Besta
Akifafanua zaidi, Mhandisi Besta amesema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni wa Barabara ya Mtwara – Newala – Masasi (km 210), ikijumuisha Daraja la Mwiti ulifanywa na Kampuni ya Mult-Tech (Pty) Ltd kutoka nchini Botswana kwa ushirikiano na Kampuni ya United Civil Consultants Ltd ya Tanzania, kwa gharama ya shilingi 1,280,831,600.00, bila kodi ya ongezeko la thamani na kazi hiyo ilikamilika Desemba, 2015
Kutokana na usanifu, sehemu isiyo na makazi, barabara hiyo imejengwa kwa upana wa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni njia ya magari na mita 1.5 kila upande ni mabega ya barabara kwa ajili ya watembea kwa miguu.
Sehemu za makazi, barabara imejengwa kwa upana wa jumla wa mita 10.5 ambapo mita 6.5 ni njia za magari na mita 2.0 kila upande ni mabega ya barabara kwa ajili ya watembea kwa miguu.
No comments