Anayeunga mifupa aiangukia Serikali
Na Omary Mngindo, Mbwawa
MKAZI wa Mbwawa, Kata ya Mbwawa Kibaha Mji Mkoa wa Pwani, Lufunga Paul, ameiomba Serikali kumuunga mkono katika kuboresha huduma anayowapatia wagonjwa wanaovunjika mifupa.
Lufunga alitoa ombi hilo mwishoni mwa wiki mjini hapa, akianza kwa kumpongeza rRis Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoiongoza nchi kwa ufanisi mkubwa, huku akigusia uboreshwaji wa sekta ya afya.
Alisema tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia, amefanya kazi kubwa ya kuboresha sekta zote ikiwemo ya afya, ambapo zahanati, vituo vya afya na hospitali zimejengwa kila kona, hali inayothibitisha ubora wa uongozi wake.
"Jambo lingine serikali kwa kututambua tunaotibu kwa kutumia miti shamba 'tiba mbadala' kupitia Wizara ya Afya, nitumie nafasi hii kuiomba serikali watuangalie kwa kutuwekea bajeti itakayotusaidia kufanya kazi zetu kwa ufanisi zaidi," alisema Lufunga.
Aliongeza kuwa, amejenga jengo lenye vyumba 10 vyenye umeme, kisima cha maji safi na magodoro wanayotumia wagonjwa wake, bado anahitaji kununua vitanda, kumalizia kuweka malumalu na dali.
"Nitumie nafasi hii kuishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowatendea haki watanzania, miradi mingi inatekelezwa kila kona, nami nikiwa mmoja wa wataalamu wa tiba ya miti shamba nimeshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya kisha kupatiwa vyeti," alisema Lufunga.
Wagonjwa Juma Sultan (Chalinze), Mussa Mgeta (Mlandizi), Miraji Rajabu (Rufiji), Seleman Juma (Kibindu) na Gidion Aron (Kigoma), walisema wanamshukuru Mwenyezi Mungu wanaendelea vizuri.
"Namshukuru sana Dkt. Lufunga anafanya kazi yake kwa weledi mkubwa, niligongwa na gari nikielekea nyumbani Kibindu, nikapelekwa hospitali, lakini akaja ndugu yangu akaniomba, nikaletwa hapa, mpaka sasa natembelea magongo, kabla ya kufika hapa hali ilikuwa mbaya sana," alisema Juma.
Sultan wa Chalinze alisema, "Nilikuwa nimebeba abiria eneo la Nero, niligongwa na gari kupoteza fahamu, nilipelekwa Kituo cha Afya, baadaye Hospitali ya Tumbi, nikaambiwa nikatwe mguu, nilikataa, nikaletwa hapa nimeungwa mfupa, leo natembelea magongo," alisema Sultan.
Naye Gidion alisema kuwa, alivunjika mguu akicheza mpira mkoani Kigoma, akapelekwa hospitali, akiwa anatibiwa akapigiwa simu na ndugu akimtaka aende Mbwawa kwa daktarihuyo kwa ajili ya kupatiwa huduma hiyo.
"Nilifika hapa Mbwawa nikaanza matibabu, namshukuru Mungu naendelea vizuri, nilivunjika mguu nikiwa nacheza mpira, lakini kwa sasa niko vizuri kwani hali yangu iko njema," alisema Gidion.
No comments