Header Ads

ad

Breaking News

Wananchi 7,000 wafikiwa na huduma ya tiba mkoba

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO), mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH), kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH

Na Mwandishi Maalum - Kilimanjaro

WANANCHI zaidi ya 7,000 wamefikiwa na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kupitia huduma ya Tiba Mkoba ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua  kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayoendelea mkoani Kilimanjaro katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH). 

Amesema JKCI imekuwa ikifanya huduma ya tiba mkoba katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambapo hadi sasa mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar imefikiwa na wananchi takribani 700 kupewa rufaa ya kwenda JKCI kwa  matibabu zaidi.

Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH), Anandumi Mmari akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG), mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH), kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema kambi hiyo ya matibabu ya moyo ni mwendelezo wa tiba mkoba ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yenye nia ya kuwafikishia wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro huduma ya tiba bobezi ya magonjwa ya moyo mahali walipo.

“Nia ya JKCI kufanya kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi ni kuhakikisha tunaendeleza ujuzi kwa wataalamu wa afya wa hapa Mawenzi na kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ambao wana magonjwa ya moyo.”

“Mwitikio katika Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa mkubwa sana, ndani ya siku mbili tayari wagonjwa 600 wamefika katika Hospitali hii kwa ajili ya kupatiwa huduma, wagonjwa wengi wanaofika tumewakuta na shinikizo la damu, na hii inatokea katika kila mkoa tunakokwenda, ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umekuwa changamoto kwa watu wengi hivyo hupata madhara ya moyo kutanuka.”

Ofisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),  Kilalo Barati akimpima shinikizo la damu mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH), kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH. Picha zote na JKCI

Dkt. Kisenge amesema JKCI itaendelea kufanya kambi hizo katika mikoa mingine iliyobaki, lengo likiwa kuendeleza dhana ya kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi pale walipo.

“Katika kambi hii pia tunatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto, kwa siku hizi mbili watoto waliofanyiwa uchunguzi wengi wao wamekutwa na matundu kwenye moyo,” amesema Dkt. Kisenge.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Dkt.EdnaJoy Munisi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Dkt. EdnaJoy amesema mwitikio wa kambi maalum ya matibabu ya moyo umekuwa mkubwa tofauti na ilivyotarajiwa, lakini timu ya wataalamu wa afya wa Mawenzi kwa kushirikiana na wenzao kutoka JKCI wamejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika Hospitali ya Mawenzi anapatiwa huduma kwa wakati na kwa ufanisi.

“Tunawaomba wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani kuendelea kufika katika Hospitali ya Mawenza kupata fursa ya kupima moyo kwani, ni fursa ya pekee hasa kwa watu wazima ambao mara nyingi hushindwa kusafiri kufuata huduma mahali zilipo,” amesema Dkt. EdnaJoy.

Naye, mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi kwa ajili ya kufanya vipimo vya moyo, Helen Kavishe, amesema furaha ya watu wa Kilimanjaro haieleziki kwa kufikishiwa huduma ya kibingwa ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambayo wengi wao hawakutarajia ingekuwa rahisi kupata huduma hiyo.

Helen alisema kutokana na wingi wa watu, imemchukuwa siku mbili kupata huduma, lakini kutokana na umuhimu wa matibabu ya moyo haikuwa shida kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kurejea tena siku ya pili ili kufanikisha matibabu hayo.

“Tunaomba huduma kama hizi wakati mwingine zipelekwe na maeneo ya vijijini ili wote tuweze kufaidika na matibabu haya ya kibingwa, kwani kiuhalisia tunaona hapa uhitaji ni mkubwa na wagonjwa ni wengi,” amesema Helen.

No comments