Wakazi wa Gumba walilia mawasiliano
Na Omary Mngindo, Gwata
WAKAZI wapatao 12,000 waishio Kijiji cha Gumba Kata ya Gwata wanaiomba Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano kuwapelekea mnara utaowasaidia kupata mawasiliano ya simu.
Wakazi hao wameliambia faharinews.co.tz kijijini hapo kwamba, wanakabiliwa na adha hiyo kwa miaka mingi, hali inayochangia kukwamisha shughuli za kimaemdeleo ukizingatia mawasiliano yanachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya uchumi.
Wakazi Joel Kifuko, Miraji Bwera na Josephine Sanga walisema kuwa, changamoto hiyo imekuwa kubwa huku wakiiomba Serikali kupitia wizara husika kuangalia namna ya kuwasaidia waondokane na tatizo hilo.
"Kwa mujibu wa sensa iliyopita, hapa Gumba tupo wakazi 12,000, tunaokabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa mawasiliano, tunaiomba serikali ituangalie na kutuondolea adha hii," amesema Joel.
Naye,Sanga amesema kilio cha mawasiliano kinachangia wananchi kushindwa kuwasiliana kwani, kuna eneo moja tu ukienda ndilo linalopatikana mawasiliano, jambo ambalo ni kero kubwa.
"Tunaathirika sana na hii hali, tunawaomba wamiliki wa makampuni ya simu watuletee minara ili nasi tuweze kupata huduma hiyo muhimu katika ulimwengu huu wa kidijitali kwani, tunataabika mno," amesema Sanga.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abdallah Changalapilo amesema adha hiyo ni kubwa hivyo, amemwomba Waziri mwenye dhamana kuangalia namna gani anavyoweza kuwasaidia wananchi hao.
"Tunashukuru kutufikia mwanaHabari, tunaimani kubwa kwamba, kero yetu hii itawafikia wakubwa hivyo watakuja kututafutia ufumbuzi, kwani adha ni kubwa hapa kijijini kwetu," amesema Changalapilo.
Diwani wa Kata hiyo, Sangaine Tikwa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, huku akieleza kuwa, tayari moja ya makampuni yamefika na kukutana na mkazi mwenye ardhi inayofaa kuwekwa mnara, hivyo adha hiyo ipo mbioni kukamilika.
No comments