Wakazi Kibwende walilia shule ya msingi
Na Omary Mngindo, Kibaha
WAKAZI wa Kitongoji cha Kibwende Kata ya Mlandizi, Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, wameeleza kilio chao cha kukosekana kwa shule ya msingi katika eneo lao.
Kilio hicho kimewasilishwa na Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mihande mbele ya Ofisa wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Juma Swalehe, wakati timu ya maofisa hao walipokuwa wakitoa elimu ya mpango wa TAKUKURU rafiki ndani ya Kata ya Mlandizi.
Amesema kuwa, kutokana na changamoto hiyo baadhi ya wazazi pamoja na kukabiliwa na changamoto ya kipato, wamelazimika kuwaandikisha watoto wao kwenye shule binafsi, kutokana na umbali uliopo.
"Katika eneo hili tunakabiliwa na tatizo la kukosa shule ya msingi ya serikali, hivyo watoto hulazimika kutembea umbali mrefu hadi Mlandizi katika Shule za JKT Ruvu na ya Mlandizi, mbaya zaidi tumezungukwa na mapori," amesema Mwalimu huyo.
Katika kikao hicho, pia kimeripotiwa changamoto ya uwepo wa matukio ya wizi uliokithiri huku wakiliomba jeshi la Polisi kuongeza doria kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake Polisi Kata, Leah Malila amezungumzia ulinzi shirikishi ndani ya maeneo yao, huku akieleza kuwa eneo la Kitemvu kulikuwa na matukio hayo, lakini kws ushirikiano wao na polisi wamedhibiti matukio hayo.
"Niwaombe tuendelee kushirikiana katika masuala ya ulinzi kwenye maeneo yetu, tuunde vikundi vya ulinzi, pia mtoe taarifa mnapoona kuna watu msiowafahamu ili tuweze kuwafuatilia kabla ya uharifu," amesema Malila.
"Niwaombe mshiriki mikutano inayoitishwa na Wenyeviti wetu, mara kadhaa wanaitisha mikutano lakini wananchi hamjitokezi," amesema Malila.
Diwani wa Kata hiyo, Euphrasia Kadala ameushukuru uongozi wa TAKUKURU kwa kufika katika kata hiyo kuwapatia elimu inayohusiana na TAKUKURU rafiki, huku akiwaomba wakazi kuzingatia elimu hiyo.
"Ndugu zangu leo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa ametuletea maofisa wake, wamekuja kutuletea elimu ya bure ambayo maeneo mengine wanaipata kwa kuisafiria na kuilipia, tuzingatie elimu hii," amesema Kadala.
Ofisa wa TAKUKURU, Juma Swalehe amewaambia wakazi hao kwamba, TAKUKURU rafiki inalenga kuwapa elimu wananchi, namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa wananchi juu ya kupambana na rushwa.
"Tunatambua kazi kubwa inayotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kila kona tunaletewa miradi yenye thamani ya mabilioni, sisi ndio wanufaika wa miradi hiyo, niwaombe tunaosimamia yuwe waadilifu kwa kununua vifaa vilivyoainiahwa kwenye miradi hisika na ai kinyume chake," alimalizia Swalehe.
Kuhusiana na changamoto zilizoainishwa na wananchi hao, Swalehe amesema kuwa wamezichukua na kwenda kuzifanyia kazi kwa wakati, kisha watarejesha mrejesho.
Katika kikao hicho kichofanyika eneo la ofisi ya Kata Kibwende, changamoto za ardhi, maji, umeme, afya, elimu na miundombonu ya barabara ziliwasilishwa na wakazi hao.
No comments