Waishukuru JKCI kwa kuwasogezea huduma za matibabu ya moyo
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Pedro Pallangyo akizungumza na mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum
ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa
JKCI na wenzao wa MRRH
Na Mwandishi Maalum – Kilimanjaro
WANANCHI wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wameishukuru Serikali kupitia
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kufikisha huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo mkoani Kilimanjaro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa
kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayoendelea katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH), wananchi hao wamesema uhitaji wa
matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo mkoani humo ni mkubwa.
Elishadai Kimaro
mkazi wa Kilimanjaro, alisema kutokana na wingi wa watu kutoka Mkoa wa
Kilimanjaro na mikoa ya jirani idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya moyo kutoka
kambi hiyo kuanza imekuwa kubwa hivyo, watu kurudishwa nyumbani na kurejea tena
siku inayofuata.
Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Parvina Kazahura akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi (Echocardiograph – ECHO) mtoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH).
“Ninaiomba Serikali huduma za matibabu ya moyo hapa mkoani
kwetu zifanyike mara kwa mara au ikiwezekana tuwe na hospitali yetu inayotoa
huduma hizi za matibabu ya moyo, kambi maalum ya siku tano na baadaye wataalamu
kuondoka haitoshelezi kufikia mahitaji ya wanakilimanjaro,” alisema Kimaro.
Kimaro alisema kupitia kambi hiyo, amepata
nafasi ya kuchunguza afya ya moyo wake kwani alikuwa na hofu ya kuwa na matatizo
ya moyo, lakini hakujua ni nini afanye hadi hapo aliposikia ujio wa madaktari
bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete hivyo naye kutumia fursa
hiyo kupima.
Twaha Masawe mkazi wa Kilimanjaro alisema huduma za matibabu ya
moyo zinazotolewa na wataalamu wa afya kutoka JKCI amezipenda kutokana na watoa
huduma wanavyozungumza vizuri na wagonjwa na kuwapa elimu ya namna ya kujikinga
na magonjwa yasiyoambukiza. Masawe alisema kupitia kambi hiyo ameelimishwa
kutokuacha kutumia dawa za shinikizo la damu na kama ataacha anaweza kupata
madhara katika moyo wake ama kupata kiharusi.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga akimsikiliza
mwananchi wa mkoa wa Kilimanjaro akijibu maswali ya ufahamu kuhusu magonjwa
yasiyoambukiza wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya
moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa Mawenzi (MRRH). Picha zote na JKCI
“Namshukuru Mungu toka nilipogundulika kuwa na shinikizo la damu nimekuwa
nikitumia dawa, kupitia elimu niliyoipata hapa nitaendelea kutumia dawa kama
inavyotakiwa sitapenda kuona napata madhara mengine ya kiafya yanayoletwa na
tatizo la shinikizo la damu,” alisema Masawe.
Naye, Isha Rashidi Mkazi wa
Kilimanjaro alisema ujio wa madaktari bingwa wa moyo Mkoani Kilimanjaro umekuwa
fursa kwake kupima moyo wake kutokana na kupenda kwake kuchunguza afya yake,
lakini pia kuna hali anazozipata mara kwa mara angependa kujua tatizo lake. Isha
alisema baada ya vipimo vya moyo kufanyika yupo tayari kupokea majibu yake na
kama atakuwa na shida ya moyo atafuata mtindo bora wa maisha ili kuweza
kuepukana na magonjwa ya moyo.
“Kuna wakati napata maumivu kwenye moyo na
kusikia mapigo yangu ya moyo kupiga kwa kasi japo si mara kwa mara, inaweza
kupita hata miezi miwili ndiyo nikasikia tena hali hii, nipo tayari kujua shida
niliyonayo na kufuata ushauri wa madaktari,” alisema Isha.
No comments