Wafugaji Ruvu walilia umeme
Na Omary Mngindo, Ruvu
JAMII ya Wafugaji wa Kata ya Ruvu mkoani Pwani inayoundwa na vijiji vya Kitomondo, Ruvu Minazi Mikinda na Ruvu Stesheni Kibaha Vijijiji Mkoa wa Pwani, wameiomba Serikali iwapelekee umeme.
Sanjali na hilo la umeme, pia wanaomba wamilikishwe ardhi watayoitumia kwa kuchimba malambo, kwani itawasaidia kuondoa changamoto za mifugo kuingiliana na wakulima wakati wanakwenda kutafuta maji.
Hayo yamo kwenye taarifa iliyoandaliwa na wafugaji hao ikisomwa na Mwenyekiti wa wafugaji kata hiyo, Michael Baruhya mbele ya waandishi wa habari, iliyoelezea mambo mbalimbali ikiwemo ya maendeleo.
"Jamii ya wafugaji tunakabiliwa na changamoto nyingi, mbali ya umeme, tunaomba tumilikishwe ardhi tutayochimba malambo, suala la umeme utatusaidia kuhifadhi maziwa na nyama," ilieleza sehemu ya ya taarifa yao.
Pia, imezungumzia uharibifu wa mazingira kutokana na jamii ya wakulima kuchoma moto maeneo ya malisho, hali inayochangia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo hayo.
"Kumekuwepo na katazo la matumizi ya maji ya Mto Ruvu, tukichimba malambo tutaokoa vyanzo vya maji, pia tunaomba daraja la kuunganisha Kitomondo na maeneo mengine," ilieleza tarifa ya Baruhya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitomondo, Ramadhani Mwiruka ameiomba serikali kumaliza mgogoro wa jamii ya wafugaji kutoka upande wa Mafidhi wilayani Kisarawe, wanaoingia kijijini humo.
"Mmoja anatokea Mafidhi na mwingine Mihugwe (majina tunayo), kila mmoja anamiliki ardhi zaidi ya ekari 200 inayoingia kijijini kwetu, hivyo wanakuja kufuata maji Mto Ruvu na kula mazao," alisema Mwiruka.
"Nawashukuru wananchi wangu kwa uvumilivu mkubwa wanaoendelea kuuonesha, kwani kinyume chake, hali ya amani na usalama ingekuwa mbaya sana," alisema mwenyekiti huyo.
No comments