Header Ads

ad

Breaking News

Wabunge 400 tumeridhia uwekezaji wa Bandari - Koka

Na Omary Mngindo, Kibaha 

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani, Silvestry Koka, amesema kuwa, asilimia kubwa ya wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameridhia kuingiwa kwa mkataba wa uwekezaji wa Bandari. 

 Koka aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa majumuisho ya ziara ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini hapa, Mwalimu Mwajuma Nyamka, ambapo alisema mchakato huo umeridhiwa na wabunge wengi.

 "Hili suala la DP World linalohusiana na mkataba wa Bandari limefika bungeni, nasi wabunge wengi wawakilishi wa wananchi tumelipitia kwa kina na kujiridhisha kwamba, ni mkataba unaolenga kuipeleka mbele nchi yetu, niwaombe wananchi tuunge mkono," alisema Koka.

 Aliongeza kwamba, "Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wana siasa wakiwashinikiza wananchi na kudai kuwa, mkataba hauna maslahi kwa nchi, niseme kwamba mkataba utakuwa na faida kubwa, tumuunge mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan," alisema Mbunge huyo.

 Alisema kuwa, katika bandari ya Dar es Salaam, huo mkataba si wa kwanza na kwamba, ukisainiwa mapato ya nchi yataongezeka maradufu hivyo, kuongeza ukamilishwaji wa miradi mingi ya kimaendeleo zaidi ya utekekezwaji unaoendelea sasa. 

 Akizungumzia shughuli za maendeleo jimboni kwake, Koka alisema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo. 

 Kwa upande wake Mwalimu Nyamka aligusia hali ya kisiasa wilayani kwake, ambapo alisema iko salama, huku akiwashukuru wanasiasa kwa kuendeleza umoja na kuwataka kumpatia ushirikiano mbunge, madiwani na wenyeviti.

 "Hali ya kisiasa iko vizuri, mbunge wetu Koka, madiwani na wenyeviti wanaendelea kuitendea haki ilani ya chama chetu, nitumie bafasi hii kuwaomba wanaosaidia chama wazingatie taratibu kwa kuwasiliana na viongozi," alisema Nyamka.

No comments