VODACOM, NMB, GOOGLE ZARAHISISHA UPATIKANAJI WA SIMU JANJA
USHIRIKIANO mpya kati ya Google, NMB na Vodacom Tanzania Plc unatarajiwa kuleta mapinduzi ya kidijitali kwa kuwezesha upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu nchini.
Kwa kulipa kiasi cha kuanzia cha Shilingi 20,000, wateja wa Vodacom wanaotimiza vigezo watapata simu janja zinazoweza kutumia mtandao wa 4G na hivyo, kunufaika na fursa zinazopatikana mtandaoni.
Mpango huo mpya uitwao 'Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo' kwa ushirikiano NMB na Android (mfumo wa uendeshaji wa Google kwa vifaa vya mkononi), unakwenda sambamba na dira ya serikali ya ujumuishi wa kidijitali.
"Maono yetu ni kuipeleka Tanzania kwenye ulimwengu wa kidijitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia, hivyo ushirikiano huu unakwenda sambamba na malengo yetu ya kuwafungulia wateja wetu fursa zinazobadilisha maisha.
Tunaamini ushirikiano huu utaleta mageuzi katika upatikanaji wa simu janja kwa wale ambao hawajanufaika na zana hizi za kidijitali.
"Tumedhamiria kuwawezesha wateja milioni moja kumiliki simu janja zenye uwezo wa 4G katika mwaka huu wa fedha pekee, hivyo kuchangia kupunguza pengo kati ya wanaotumia na wasiotumia intaneti nchini," amesema Hilda Bujiku, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Mikopo ya simu ni mbinu inayowezesha umiliki wa simu janja kirahisi na kwa gharama nafuu kupitia malipo ya siku au ya wiki kwa kima kidogo cha hadi sh.900, huku mtumiaji akifurahia manufaa yanayokuja na kuunganishwa kidijitali.
Ushirikiano huu utatumia uwezo mpya wa kipengele cha kusimamia vifaa kwenye mfumo wa uendeshaji wa Android.
“Lengo la Android daima limekuwa kuwawezesha watu kupitia huduma za kikompyuta. Ufikiaji wa fursa zilizo kwenye intaneti ni muhimu sana kwa ukuaji wa kiuchumi na ujumuishaji wa kijamii katika nchi yoyote ile.
"Tunaamini kwamba ushirikiano huu utawaleta Watanzania wengi mtandaoni na kuwasaidia kutumia fursa zinazopatikana mtandaoni,” amesema Martin Njoroge, Mkuu wa Android wa Ushirikiano wa Kimajukwaa, Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Benki ya NMB,Filbert Mponzi, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo, amesema, “Ubia huu wenye tija ni sahihi kabisa kwani Vodacom itawapatia wateja wake mpango wa kulipia simu janja hivyo, kuwezesha kupanda daraja na kumiliki simu janja kupitia malipo ya awamu hivyo kufungua uchumi wa kidijitali na kutengeneza fursa za ziada kwa Watanzania.
Vile vile, ubia huu unakuwa sambamba na ajenda yao ya ujumuishwaji wa kidijitali maarufu Teleza Kidijitali.
Kufurahia huduma hii, wateja wa Vodacom watatakiwa kupiga *150*00# > 5 > 5 > 1 # ili kuona kama wanakidhi vigezo na hivyo kujiunga kwenye huduma, baada ya hapo watapokea SMS iliyo na namba ya kumbukumbu. Wateja watachukua simu zao katika maduka ya Vodacom baada ya kulipa kianzio cha hadi Shilingi 20,000.
Vodacom itawazawadia wateja wake MB 100, dakika 10 za kupiga mitandao yote na SMS 10 zitakazotumika ndani ya saa 24, pindi watakapokamilisha marejesho kwa wakati.
Ikiwa mteja hatafanya marejesho kwa wakati, Vodacom itafunga kifaa hicho, hata wakati simu imefungwa mteja atawasiliana na huduma kwa wateja, kutumia M-PESA pamoja na aplikesheni ya Kiosk.
Kwa maelezo zaidi kuhusu Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo, wateja wa Vodacom wanahimizwa kubonyeza *150*00# > 5 > 5 > 6 au kupiga namba ya huduma kwa wateja kupitia nambari 100 ili kupata maelezo zaidi.
No comments