Header Ads

ad

Breaking News

TUME YA UCHAGUZI YATAO VIBALI VYA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA MBARALI

 Na Mwandishi wetu, Dodoma.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa ubunge Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara kwa asasi tatu za kiraia.

Taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Tume kukutana katika kikao chake leo Agosti  17,2023 jijini Dodoma.

“Tume imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kifungu cha 4C cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na kanuni ya 3 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020, inayoipa Tume jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kailima amezitaja asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na maeneo watakayotoa elimu hiyo ni Alpha and Omega Reconciliation and Peace Building (AREPEB),  itakayotoa elimu hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwenye Jimbo la Mbarali.

Nyingine ni Umbrella of Women and Disabled Organisation (UWODO), itakayotoa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ndani ya Kata ya Mtyangimbole na Bright Child Development Tanzania (BRIGHT CHILD), ambayo itatoa elimu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Kata ya Mwaniko.

Tume hiyo imetoa kibali cha utazamaji kwa Asasi ya kiraia ya Bridge Development Trust Organization (BRIDETO), ambayo iliomba kutazama uchaguzi mdogo katika Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kailima katika taarifa hiyo amesema kuwa, Tume imefikia uamuzi wa kutoa kibali hicho kwa kuzingatia kanuni ya 16(5) ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani), za mwaka 2020

Mkurugenzi huyo amesema katika utekelezaji wa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura, asasi hizo zitapaswa kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020 katika kipindi chote cha kutoa elimu hiyo katika uchaguzi mdogo.

No comments