PETER MWENDA AFARIKI DUNIA, TASWA WATUMA SALAMA ZA POLE
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa kiongozi wa zamani wa TASWA, Peter Mwenda aliyefariki dunia alfajiri ya leo Agosti 16, 2023 jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TASWA, Alfred Lucas imeeleza kuwa, chama hicho kimepoteza mtu mahiri katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.
“Tunatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki, waandishi wa habari za michezo na wanamichezo wote kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa.
“Tutaendelea kumkumbuka Mzee Mwenda kwa mambo mbalimbali ambayo aliyafanya wakati wa uhai wake katika kuimarisha chama chetu na tasnia ya tasnia ya habari kwa ujumla.
“Tunaungana na wote wanaomboleza kwa ajili ya kifo chake, kumwombea apate pumziko la milele,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Mwenda enzi za uhai wake aliwahi kufanhyakazi katika Kampuni ya Business Times Limited (BTL), iliyokuwa ikichapisha magazeti ya Majira, Business Times, Spoti Starehe, Dar Leo, Maisha, Mwanamke, Daily Times, Sanifu na Alwatani.
Mkongwe huyo katika miaka ya nyuma aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA kwa vipindi vitatu.
No comments