MWENYEKITI TEF AMPONGEZA MKURUGENZI IDARA YA HABARI KWA KAZI NZURI
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amempongeza Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),Gerson Msigwa kwa kazi nzuri ya kuingilia kati maeneo ambayo maofisa wa serikali walikuwa wakitaka kuwanyanyasa wanahabari.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 17,2023, katika ofisi za TEF, jijini Dae es Salaam, Balile amesema, baadhi ya maofisa wa serikali walitaka kuendelea na utamaduni wao wa kunyanyasa waandishi wa habari, lakini jambo hilo limekuwa likiingiliwa kati na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Msigwa.
“Wapo maofisa wa serikali waliotaka kuendeleza utamaduni wao wa kunyanyasa waandishi wa habari, lakini nimshukuru Msigwa, kwani amekuwa makini kuhakikisha anadhibiti tabia hiyo,” amesema Balile.
Balile ashauri Wizara ya Habari kuhakikisha inakamilisha uundaji wa kanuni za habari hadi ifikapo Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa, jukumu la kusimamia na kukamilika kwa kanuni hizo ni la Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Amesema wanapenda kanuni za habari zikamilike Oktoba mwaka huu, huku akisisitiza hilo ni ombi kwa kuwa, Waziri wa Habari, Nape Nnauye, halazimishwi na sheria kuhusisha wadau.
“Kutokana na utaratibu wake wa kushirikisha wadau ndiyo maana anafanya hivyo, wakati huu suala la kanuni za habari linaishia kwa kwake Waziri Nape, halipelekwi bungeni,” alisema.
Balile amesema, baada ya bunge kupitisha marekebisho ya sheria ya habari, sasa ni kuomba fursa ya kukutana na serikali kwa ajili ya kupendekeza mambo gani yaingie kwenye kanuni.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo wadau wa habari wangependa yaingie kwenye kanuni mpya na kuanza kutumika ni suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano, tofauti na ilivyo hivi sasa.
Mwenyekiti huyo wa TEF amesema wataishauri serikali kuwa, kanuni zielekeze leseni pamoja na kitambulisho cha mwanahabari (press card), vidumu kwa zaidi ya miaka mitano.
“Makosa ya kitaaluma yanapaswa kubaki kwa wanataaluma wenyewe, hili litasaidia sana kupunguza kesi nyingi mahakamani.”
Balile amesema, eneo lingine wanalotarajia liingie kwenye kanuni, ni umiliki wa hisa katika vyombo vya habari kutowekewa mipaka.
"Siyo jambo rahisi kwa mwekezaji kutoka nje kuwekeza kwenye vyombo vya habari, asiwe na sauti, huku akitoa mfano wa uwekezaji wa bila kiwango cha asilimia katika maeneo mengine ikiwemo mitandao ya simu,"amesema.
Balile amesema sheria inataka mwekezaji kutoka nje ya nchi amiliki hisa isiyozidi asilimia 49, jambo ambalo linapunguza uwekezaji kwenye vyombo vya habari.
“Tutamshauri Waziri Nape kwamba, mwekezaji kwenye vyombo vya habari asiwe na ukomo kama ilivyo kwenye mitandao ya simu na maeneo mengine,” amesema.
Ameongeza kwamba,miongoni mwa sehemu ya sheria ya sasa inaruhusu mwandishi wa habari kumshitaki mtoa taarifa endapo atakataa kutoa taarifa inayotakiwa na mwanahabari.
“Hili lieleweke vizuri, kuna maofisa wa serikali ambao wakitakiwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari, hugoma kufanya hivyo, kwa sheria ya sasa mwanadishi wa habari anaweza kumpeleka mahakamani ofisa ambaye atakataa kutoa taarifa inayotakiwa,” amesema Balile.
No comments