MKUU WA MKOA DAR AVUNJA UONGOZI SOKO LA NDIZI-MABIBO
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Agosti 17,2023 amevunja uongozi wa Soko la Mabibo na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanya uchunguzi wa kina katika soko hilo na watakaobainika kukiuka maadili ya uongozi, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Chalamila ametoa kauli hiyo katika soko hilo wakati akitatua mgogoro kati ya wafanyabiashara wasio waaminifu wakiongozwa na uongozi wa soko hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Mkuu wa Mkoa amekemea watu wachache, wabinafsi katika soko hilo kukwamisha jitihada za serikali, huku akionya kwamba kamwe wasijaribu hata kidogo.
Amesema masoko lazima yaboreshwe ili Serikali ikusanye mapato yake na wafanyabishara wafanye biashara zao sehemu rafiki.
"Hatuwezi kuacha watu wachache wajinufaishe na serikali inakosa mapato, Mkurugenzi wa Manispaa anza kazi leo," Amesema Chalamila.
Hata hivyo, Chalamila amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, dhamira yake ni kuboresha masoko,na tayari kiasi cha shilingi milioni 600, kimetengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya kuanza kuliboresha Soko hilo.
Mkuu wa Mkoa amesema uongozi uliokuwepo ulikuwa ukikusanya fedha nyingi, lakini zilikuwa zikiishia katika matumbo ya watu wachache, badala ya kuwanufaisha walio wengi, ambapo alikiri wazi kutokubaliana nalo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba ameweka wazi Changamoto zilizoko katika Soko hilo na kuonesha dhamira ya Wilaya yake kutaka maboresho ya Soko hilo muhimu kwa masilahi mapana ya Umma.
Amesema ni kweli mmiliki halali wa soko hilo ni Urafiki ambao walikaa na kukubaliana kuendeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo hivyo, tayari manispaa imetenga shilingi millioni 600 ili kuanza Ukarabati wa Soko hilo.
No comments