Milioni 100 zatolewa matibabu ya moyo kwa watoto
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.
Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge hundi ya shilingi milioni 100 iliyotolewa
katika Viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es Salaam na Benki ya CRDB. fedha
hizo zimekusanywa kwa washiriki wa mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya
kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Dkt. Hussein alisema panapotokea wadau kama benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB Marathon kusaidia sehemu iliyobaki katika ruzuku ya masuala ya afya hupunguza jukumu la serikali ambayo ingelazimika kubeba mzigo wote.
Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Shilingi Milioni 100 zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio za
CRDB Marathon msimu wa nne kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi
vilivyopo Oyster bay jijini Dar es Salaam Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema Serikali imekuwa ikitoa
ruzuku ya zaidi ya asilimia 80 kuchangia gharama za matibabu ya magonjwa
mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
Dkt. Hussein alisema panapotokea wadau kama benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB Marathon kusaidia sehemu iliyobaki katika ruzuku ya masuala ya afya hupunguza jukumu la serikali ambayo ingelazimika kubeba mzigo wote.
“Nimefurahi kusikia mbio hizi zinaendelea kuwasaidia watoto wetu kupata
huduma za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani
imekuwa ikifanya kazi nzuri kutibu watanzania wenye changamoto ya magonjwa
ya moyo kutoka pande zote za nchi yetu”, alisema Dkt. Hussein.
Dkt. Hussein alisema bado zipo familia nyingi ambazo hata asilimia tatu zinazobaki
baada ya ruzuku kutolewa na serikali hazina uwezo wa kumudu gharama za
matibabu yakiwemo magonjwa ya moyo hivyo kuwaomba wadau kuendelea
kutafuta fedha kusaidia watu kupata matibabu hayo.
“Bado mahitaji katika sekta ya afya ni makubwa hivyo ni jambo la faraja kwetu
kupata mchango huu wa mbio za CRDB ambao unasaidia kuongeza nguvu kufikia
malengo yaliyopangwa na Serikali”, alisema Dkt. Hussein.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),
Dkt. Peter Kisenge ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa
kuwasaidia watoto ambao wanatibiwa katika Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema Benki ya CRDB kwa miaka minne mfululizo imekuwa sehemu
ya kurejesha tabasamu kwa watoto ambao wanatoka katika mazingira magumu
hivyo kushindwa kugharamia matibabu lakini kupitia mbio hizo watoto
wamekuwa wakipatiwa matibabu.
“Gharama za matibabu ya moyo ni kubwa, hii inatokana na vifaa vinavyotumika
kuwa na gharama kubwa, kupitia mbio za CRDB Marathon watoto wanaotoka
katika mazingira magumu hupata nafasi ya kutibiwa magonjwa ya moyo”, alisema
Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema
Benki ya CRDB itaendelea kuzifanya mbio za CRDB kuwa endelevu kwa maslahi
mapana ya jamii na Taifa.
Abdulmajid alisema Mbio za CRDB kwa mwaka 2020 zilichangia fedha kwa ajili ya
upasuaji wa moyo kwa watoto 100, mwaka 2021 pia walichangia fedha za
upasuaji wa moyo kwa watoto 100, na mwaka 2022 zilichangia fedha kwa ajili ya
upasuaji wa moyo kwa watoto 125.
“Mwaka huu CRDB Marathon inatoa fedha milioni 100 kwa ajili ya watoto wetu
wanaotibiwa JKCI tukiendelea kuwarejeshea tabasamu watoto wenye magonjwa
ya moyo ambao wamekuwa wakihitaji msaada kufanikisha matibabu yao”,
alisema Abdulmajid.
Msimu wa nne wa mbio za CRDB Marathon umelenga kuchangia matibabu ya
watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete, kujenga kituo cha afya ya mama na mtoto visiwani Zanzibar, kuchangia
matibabu ya akina mama wenye ujauzito hatarishi na changamoto ya Fistula
wanaotibiwa CCBRT, pamoja na kuwekeza katika programu ya kuipendezesha
Tanzania kwa kuimarisha bustani za Zanzibar.
No comments