Mafanikio yametokana na mshikamano wetu-Ridhiwani
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete
Na Omary Mngindo, Chalinze
NAIBU Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, amesema mafaniko yanayoendelea kupatikana jimboni humo yanatokana na mshikamano mkubwa uliopo kati ya viongozi na wananchi.
Ridhiwani alitoa kauli hiyo kwa wananchi wa maeneo ya vijiji na vitongoji vinavyounda Kata ya Talawanda jimboni hapa, akiwa kwenye ziara ya siku moja ya kukagua shughuli za maendeleo kwenye vijiji vya Msigi, Magulumatali na Mindukene.
"Ndugu zangu wana Talawanda na jimbo zima la Chalinze kwa ujumla nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa namna tunavyoendelea kushirikiana katika shughuli za maendeleo, umoja wetu ndiyo ushindi," amesema Ridhiwani.
Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa anazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha nchi inazidi kupiga hatua katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Ramadhani Biga amewapongeza madiwani wenzake kwa mshikamano unaondelea kati yao, Mbunge Ridhiwani na wa Viti Maalumu, Subira Mgalu, kwa kazi kubwa wanayofanya jimboni humo.
"Kwa niaba ya wana Talawanda, kipekee kabisa nimpongeze na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge Ridhiwani, Mgalu, mwenyekiti wa halmashauri, mkurugenzi, madiwani wenzangu na wataalamu wote, Talawanda miradi inaendele kuletwa," amesema Biga.
Katika ziara hiyo, Ridhiwani ametekeleza ahadi yake ya kuchangia mabati kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za chama katika kata hiyo.
No comments