Kinana: Uhuru wa kusema uwe na mipaka
NA MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema pamoja na nchi kuwa na uhuru mkubwa wa kusema na kutoa maoni, lakini kikubwa kinachotakiwa ni kuzingatia mipaka.
Akizungumza jijini Dar es Sa,laam Agosti 22,2023, katika mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Kinana amesema uhuru wa kusema ni mkubwa, lakini kila uhuru una mipaka yake.
Amesema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa akiwafundisha kuwa, uhuru bila ya nidhamu ni wendawazimu na nidhamu bila ya uhuru ni utumwa, hivyo kila uhuru unatakiwa uwe na mipaka yake, hivyo uhuru upo wa kutosha, labda kama kuna kasoro katika utekelezaji wake, ndio maana Watanzania wanapiga kelele katika kusimamia sheria zinazowapa Watanzania uhuru wa kusema.
Akizungumzia katiba mpya na haki katika uchaguzi, Kinana amesema jitihada zimekuwa zikifanyika kwa muda mrefu katika awamu mbalimbali, lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira na kutekeleza kwa vitendo kuhakikisha inafanikiwa.
“Kuna hili jambo la katiba, kumekuwepo na jitihada nyingi sana, kumekuwepo na tume nyingi, kumekuwa na Tume ya Nyalali, Tume ya Kisanga na Tume ya Warioba, zote hizi ni juhudi za kutafuta Tanzania kuwa na katiba nzuri, katiba itakayowapa Watanzania uhuru wa kuamua kushiriki mambo yao kwa uhuru.
“Lazima nikiri kwamba, awamu hii tangu imeingia madarakani juhudi zimeanza kufanyika, hata wakati Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa baraza la vyama vya siasa, mkutano wa kituo cha Demokrasia (TCD) na hata alipokuwa akifungua mikutano ya hadhara, alisema jinsi serikali ilivyojipanga kuhakikisha tunakuwa na katiba na hata sasa hivi kuna mchakato wa aina mbili unafanyika.
“Mchakato wa kwanza ni wa kutafuta namna ya kupata katiba, lakini kwa sababu mchakato huu utachukua muda kuna mchakato wa pili ambao ni wa kurekebisha maeneo matatu ambayo yanahusu uchaguzi, huu ni kwa ajili ya uchaguzi wa 2024 na 2025,” alisema.
Alisema sheria hizo tatu zitatazamwa upya ili zijibu matakwa ya hali halisi ya demokrasia kwa hali ya sasa.
“Ya kwanza ni sheria inayohusu tume ya uchaguzi, yapili ni sheria inayohusu uchaguzi wenyewe utakavyoendeshwa nay a tatu ni sheria inayohusu namna vyama vya siasa vitakavyosimamiwa.
"Mimi nina hakika sheria hizi tatu zikitazamwa na sote kwa pamoja tukikubaliana kupitia vikao kama hivi kupitia TCD na baraza la vyama nina hakika tutakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki zaidi kuliko wakati wowote mwingine kutoa nafasi kwa Watanzania kuwachagua wale ambao wangependa wawe wawakilishi katika vyombo vya uwakilishi."
“Kwa hiyo je, demokrasia imekuwepo, mimi naamini naam imekuwepo kwa kutazama namna idadi ya wawakilishi wa vyama ilivyokuwa ikiongezeka, je kuna kasoro, naam kasoro zipo na ndio mana tunakutana humu ndani na tutakutana katika baraza la vyama kushughulikia kasoro hizo kuzisahihisha, je dhamira kwenye awamu hii ipo, naam nadhani dhamira ipo na ni muhimu kushirikiana tufikie dhamira hiyo, tupate sheria nzuri na hasa sheria zinazosimamia uchaguzi, tume ya uchaguzi na sheria ya vyama ili uchaguzi ujao wa 2024/2024 uwe wa haki zaidi,” amesema.
Fullshangwe blog.
No comments