Kibaha Vijijini yaanza ujenzi wa sekondari ya sita
Na Omary Mngindo, Kitomondo
SEKONDARI ya sita imeanza kujengwa ndani ya Jimbo la Kibaha Vijijini mkoani Pwani, katika Kitongoji cha Kisabi, Kata ya Mtongani jimboni hapa.
Ujenzi huo ulianza kwa kuchimba msingi, ni sekondari ya sita ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu ya Rais Samia Suluhu Hassan, chini ya Mbunge Michael Mwakamo akisaidiana na madiwani wa kata zinazounda jimbo hilo.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mbunge Mwakamo akiwa katika Kijiji cha Kitomondo, muda mfupi baada ya dua ya kuwarehemu wazee waliotangulia mbele ya haki, utaratibu aliouanzisha kila mwaka.
"Naishukuru serikali inayoongozwa na rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha miaka miwili na nusu, ndani ya jimbo letu tayari tuna sekondari sita na zahanati sita, pia niwashukuru wana Kibaha Vijijini kwa kuendelea kunipa ushirikiano," alisema Mwakamo.
"Naendelea kupigania maendeleo ya wananchi, ndiyo maana ninapomuona mtu analeta siasa katika maisha ya watu, ninachukia sana, nayafanya haya bila ya kuangalia matokea ya mwaka 2025," alisema mbunge huyo.
Alisema atahakikisha ifikapo mwaka 2025, kata zote zitakuwa na sekondari, huku akiweka wazi kuwa, amebakiwa na Kata za Mtambani, Janga, Ruvu na Dutumi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ruvu, Shaabani Chamba alimwambia mbunge huyo kwamba, wametenga ardhi ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari na kituo cha afya cha kata hiyo.
No comments