Header Ads

ad

Breaking News

Jumaa ataka viwanja vya michezo Mlandizi


Na Omary Mngindo, Mlandizi

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Jumuiya ya Wazazi Taifa, Humoud Jumaa, amewataka viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuelekeza mawazo yao kwenye ujenzi wa viwanja vya michezo.

Jumaa ametoa kauli hiyo kwenye hafla maalumu ya Simika Bendera kwenye Kata ya Mtambani, ambapo amesema atawasiliana na viongozi hao ili kufanikisha kupatikana kwa moja ya eneo litalotumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanja hivyo.

Ameongeza kwamba, Mji wa Mlandizi unaendelea kukua kwa kasi, lakini hauna eneo linalowapatia fursa watoto kushiriki michezo, sanjali na kwa watu wazima kujumuika kwenye mashindano mbalimbali, hali inayotakiwa kuangaliwa kwa jicho la kipekee.

"Mlandizi tuna maeneo mawili, kwa Mama Salmini ambalo limeshanunuliwa na halmashauri yetu kwa ujenzi wa soko, pia pale bondeni kulikotaka kujengwa soko na stendi, lakini naona kwa viwanja vya michezo sehemu nzuri ni kwa Mama Salmini," amesema Jumaa.

Ameongeza kwamba, kukiwa na viwanja wananchi watakuwa na muda wa kushriki michezo,kubadilishana mawazo na kujenga afya.

"Kwa soko pale kwa Mama Salmini naona kutakuwa na changamoto ya magari, hii inatokana na ufinyu wa barabara ukilinganisha na magari yatakayotakiwa kupeleka mizigo, hivyo kwa viwanja vya michezo patafaa sana," amesema Jumaa.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo, wananchi baada ya shughuli za ujenzi wa taifa wanapaswa kuwa na muda wa kushiriki michezo.

No comments