Jumaa ataka Koka aachwe afanye kazi
Na Omary Mngindo, Kibaha
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Jumuiya ya Wazazi Taifa, Humoud Jumaa, amewataka wanachama na wadau na chama hicho kumpa nafasi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka afanye kazi yake.
Jumaa aliyasema hayo katika majumuisho ya ziara ya Mwenyekiti wa chama hicho Kibaha Mji, Mwajuma Nyamka, ambapo amesema kwa miaka mingi chama hicho kimekuwa kikisaidiwa na wanachama wakiwemo wadau, lakini wanafuata taratibu za kuwasiliana na viongozi ngazi mbalimbali.
"Chama chetu kimekuwa kikisaidiwa na wana CCM wenyewe kuanzia wazee wetu hadi sasa tunafanya hivyo, lakini ni jambo la busara tufuate taratibu kwa maana ya kuwasiliana na viongozi wetu ngazi mbalimbali, hata mimi nasaidia Kibaha vijijini, nafuata taratibu," amesema Jumaa.
Awali, Mwenyekiti wa chama hicho mjini hapa, Mwajuma Nyamka aliwaonya wanasiasa wanaosaidia kwa kutofuata taratibu, huku akisisitiza kwamba, uongozi wake hautakuwa tayari kuona siasa inavurugwa.
"Kwa sasa mbunge wetu bado ni Koka na madiwani waliochaguliwa kwenye uchaguzi uliopita, hivyo sitakuwa tayari kuona wanachama wenzetu wanafanya fujo," amesema Nyamka.
Silvestry KokaAkizungumza na mamia ya wana CCM wa Kibaha Mji, Mbunge wa jimbo hilo, Koka alizungumzia mchakato wa uwekezaji wa Bandari, kwamba wabunge zaidi ya 400 wameridhia mchakato huo wa uwekezaji.
"Bandari yetu si mara ya kwanza kuwa chini ya mwekezaji, kwa miaka kadhaa ipo chini ya kampuni ya TICS, lakini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona utendaji usioridhisha akaamua kutafuta mwekezaji mwingine ambaye ni DP World," amesema Koka.
"Mchakato wake bado unaendelea, niwaombe watanzania tuungane na Rais wetu kuhakikisha malengo yake ya kuhakikisha nchi inaendelea katika nyanja mbalimbali," amemalizia Koka.
Mwajuma Nyamka
No comments