Header Ads

ad

Breaking News

JKCI kushiriki Kongamano la Dunia la wataalam wa magonjwa ya moyo nchini Marekani


Na Stella Gama, Dar es Salaam

MADAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto watano kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), watashiriki Kongamano la nane la Dunia la watoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto linalofanyika nchini Marekani.

Kongamano hilo limepangwa kuanza Agosti 28,hadi 3 Septemba 2023, ambapo jumla ya washiriki zaidi ya 4,500 kutoka nchi mbalimbali duniani watashiriki.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Daktari bingwa wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya JKCI, Naizhijwa Majani alisema kongamano hilo hufanyika kila baada ya miaka minne, ambapo mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2017 jijini Barcelona nchini Hussein.

“JKCI iliweza kushiriki katika kongamano la saba lililofanyika nchini Hispania na kujifunza kuhusu msingi wa data shirikishi wa uboreshaji wa ubora wa huduma kimataifa (International Quality Improvement Collaborative Data Base - IQIC), inayosaidia kuangalia masuala ya ubora kwenye huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.”

“Baada ya kujifunza tulianzisha hapa JKCI data base hiyo na hadi sasa Tanzania ni kati ya nchi tatu za Afrika zinazotumia data base hiyo inayosimamiwa na wataalam waliopo Boston,” amesema Dkt.Naizhijwa.

Dkt. Naizhijwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa Huduma JKCI, amesema kupitia data base hiyo, JKCI inapeleka taarifa zote za upasuaji wa moyo unaofanywa, maendeleo ya wagonjwa, aina ya upasuaji unaofanywa na kulinganishwa na wenzao wa Afrika na nchi nyingine nje ya Afrika.

Aidha, Dkt. Naizhijwa amesema katika kongamano la nane, wataalam wa JKCI  wameweza kutuma majalada 9 ili yaweze kutumika, ambapo majalada saba yamekubaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kongamano hilo.

“Ni nafasi ya kipekee kwetu kwani majalada hadi yaweze kukubalika kuwasilishwa katika kongamano hili la kipekee kwa watoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto, lazima yakidhi viwango vinavyohitajika.”

“Kupitia kongamano hili, JKCI inapeleka kazi zake ili ziweze kuonekana na kuitangaza taasisi, kutengeneza uhusiano na wataalam kutoka nchi mbalimbali duniani, kufungua fursa za masomo, utafiti na kubadilishana uzoefu,” amesema Dkt.Naizhijwa.

No comments