Header Ads

ad

Breaking News

Dkt.Biteko:Maonesho ya madini yataufungua kiuchumi Mkoa wa Lindi

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko

MAONESHO ya Kwanza ya madini na fursa za uwekezaji yanayoendelea mkoani Lindi, yametajwa kuufungua mkoa huo kiuchumi na kuongeza fursa uwekezaji katika Sekta ya madini.

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko, amezungumza na wadau wa sekta ya madini wanaoshiriki maonesho leo Agosti 25, 2023.

Amesema maonesho hayo yamewakutanisha wadau wa Sekta ya madini kutoka nchi zaidi ya 10, waliofika nchini kujifunza   na kuangalia fursa za uwekezaji mkoani Lindi.

Wageni walioshiriki maonesho hayo wametoka China, Marekani, Canada, Australia, Japan, Sri Lanka na Finland.

“Naomba kutoa wito kwa wananchi wa Lindi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji watakaofika kuwekeza nchini ili tunufaike na uchimbaji wa rasilimali madini,” amesema Dkt.Biteko.

Dkt.Biteko amesema kuwa, shughuli na biashara katika Sekta ya madini zifanywe na Watanzania wenye sifa ili wazawa wanufaike na uchumi wa madini na kuongeza mchango wa Sekta katika pato la taifa.

Meneja wa Huduma ya Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Solomon Maswi amesema GST imechora ramani ya jiolojia ya Mkoa wa Lindi na nchi nzima kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kuanzia ngazi ya mkoa na nchi nzima ambayo inapatikana kwa lugha ya Kiswahili.

Maswi amesema kuwa, GST imefanya Utafiti wa awali na kuja na mapendekezo ya madini mkakati 31 na madini muhimu 11 kwa nchi nzima.

Amesema Mkoa wa Lindi una madini mkakati sita ambayo ni chuma, Kinywe, dhahabu, shaba, magnesite na manne muhimu ambayo ni jasi, chokaa, chumvi na Chuma.

Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt.Venance Mwasse, amesema shirika hilo limetekeleza majukumu mbalimbali, hususan ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha chumvi ili kupata soko la uhakika mkoani Lindi.

Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Lindi, Mhandisi Iddi Msikozi amesema lengo la maonesho ya Madini mkoani humo ni kuonesha dunia kwamba, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali madini za kutosha na wadau wamekaribishwa kuwekeza katika mkoa huo ili Watanzania wanufaike na uchumi wa madini.

Wengine waliotoa mada katika maonesho ni Kamishna wa Madini Dkt.AbdulRahman Mwanga, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Hassan Ngoma, Mjiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt.Japhet Fungo, Mjiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Yunnan Prof. Xuance Wang na Katibu Mkuu Umoja wa Wachimbaji wa Madini (UVIWAMA), Castory Mtonga.

No comments