Header Ads

ad

Breaking News

ATCL, NMB WAZINDUA USHIRIKIANO

BENKI ya NMB na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamezindua ushirikiano wa kibiashara wa mifumo ya malipo ya tiketi za ndege 'Anga Rafiki - Tiketi Yako Imebima,' unaowapa fursa wasafiri wa kulipia tiketi kupitia matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi App, ambazo zitakuwa zimekatiwa Bima ya Safari moja kwa moja.


Ushirikiano huo umezinduliwa Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam  Agosti 16, 2023, wakati msafiri atakayelipia tiketi za safari za ndani ya nchi kupitia NMB, atakatiwa bima ya maisha, ulemavu ama upotevu wa mizigo safarini, ambayoitamwezesha kulipwa hadi shilingi milioni 5, itapotokea mteja kufariki dunia.

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ruth Zaipuna, amesema kupitia matawi yake 229 na mawakala zaidi ya 21,000, wasafiri nchini watafikiwa kirahisi kuwezeshwa upataji tiketi, ambapo wateja wa benki hiyo wanazo njia za ziada za kulipia tiketi kwa simu ya mkononi kupitia USSD na NMB App.

"Imani yetu NMB kuwa, huduma hii si tu itampa urahisi msafiri kulipia tiketi yake, bali itamkinga na majanga yatokanayo na safari kama ulemavu, kifo na upotevu wa mizigo.

"Mteja akilipia tiketi ya ATCL kupitia NMB, ikitokea amefariki, (hatuliombei hilo),  ama kupata ulemavu akiwa safarini, yeye ama wategemezi wake watalipwa hadi shilingi milioni 5.

"Ikiwa mzigo (checked in Baggage) wa msafiri utapotea, mteja atalipwa shilingi 300,000, pia ikiwa safari itasogezwa ama kuahirishwa, atalipwa shilingi 150,000. Bima hizi tutazilipa kupitia washirika wetu Kampuni ya Reliance Insurance," amesema Zaipuna.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, ameipongeza NMB kwa ushirikiano wao, kuweka ziada ya Bima ya Safari kwa wateja wao, na kwamba  hakuna tena sababu ya watanzania kusafiri kwa hofu wakati kuna ATCL na NMB.

"ATCL kila siku tunajikita kuboresha utoaji huduma zetu, kuanzia tiketi inapokatwa, mteja anapokuwa safarini hadi kufika, hivyo tunajivunia ushirikiano wetu na NMB, utasaidia kututofautisha na watoa huduma za usafiri wa anga wengine."


Matindi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uwezeshaji inaowapa katika kutoa huduma kwenye Sekta ya Usafiri wa Anga kitaifa na kimataifa, kufikia mwakani watatanua mtandao wa ndege zao kufikia 16.

Aliitaka NMB kujiweka tayari kuhudumia wateja wa ndege zao hizo, ikiwamo kujenga mazingira ya kuongeza chachu ya usafirishaji wa mazao na bidhaa za ndani kwenda nje ya nchi.

No comments