MKURUGENZI MPYA WA UBA AAHIDI BENKI YAO KUENDELEA KUISAIDIA SERIKALI KATIKA MIPANGO YA MAENDELEO
Na Said Mwishehe
UONGOZI wa United Bank for Africa(UBA) Tawi la Tanzania umeweka wazi moja ya mkakati wake ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza mipango ya maendeleo huku ukisisitiza kutoa huduma bora za kibenki nchini.
Pia umesema unajivunia mafanikio yake katika kutoa huduma bora za kibenki na uwepo wake nchini Tanzania umetoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuendelea kueleza namna ambavyo wamekuwa wakitoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, wakubwa na wakati.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam wakati wa kutambulishwa kwa Mkurugenzi mpya wa Benki hiyo nchini Usman Isiaka ambapo uongozi wa UBA umetumia nafasi hiyo kuelezea mipango mbalimbali na hatua ambazo wanazoendelea kuchukua katika kutoa huduma bora kwa wateja wao.
Akizungumza kuhusu ushirikiano kati yao na Serikali mbele ya waandishi wa habari Isiaka amesisitiza umelenga katika kusaidia miundombinu ya barabara, nishati, elimu na kukuza mitaji ya wajasiriamali.
"Tunajivunia kuwepo nchini Tanzania na kwetu ni fahari kubwa tunapoona tunatoa huduma za kibenki lakini wakati huo huo tunashiriki katika kusaidia ukuaji wa maendeleo katika nyanja mbalimbali.Hivyo tutaendelea na mkakati huo kwani UBA ipo kwa ajili ya Bara la Afrika ikiwemo na Tanzania,"amefafanua.
Ameongeza kwa kuzingatia taratibu na misingi ya uendeshaji wa huduma za kibenki nchini, UBA imejipanga kuhakikisha inawasimamia wajasriamali wadogo na wakubwa pamoja na kampuni kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu, ili kukuze mitaji na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi ambao umeendelea kuwa imara siku hadi siku .
Kuhusu benki hiyo amesema inafanya shughuli zake katika nchi 20 za Bara la Afrika na kubwa zaidi wamejiimarisha katika utoaji wa huduma bora za kifedha nchini huku ikikusudia kuendeleza mikakati katika maendeleo ya sekta za kilimo,nishati, barabara pamoja na uzalishaji wa bidhaa za viwanda.
Wakati kwa Tanzania, amesema tangu ianzishwe miaka tisa iliyopita UBA imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali na kusaidia kusukuma kasi ya ukuaji wa maendeleo ya nchi, hatua inayowafanya wao waaamini wanatekeleza wajibu wao.Isiaka ameipongeza Tanzaniakwa namna inavyozisimamia taasisi za kibenki licha ya uwingi wa taasisi hizo hapa nchini
Wakati huohuo Ofisa Mtendaji Mkuu wa UBA Kanda ya Afrika Mashariki Emeke Iweriebor, amesema pamoja na maboresho ya huduma mbalimbali yanayofanywa na benki hiyo kwa wateja wake, wamekusudia kuendelea kufungua matawi maeneo mbalimbali hapa nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja wake.
Pia wamewaomba watanzania kuendelea kujiunga na UBA ili nao wawe sehemu ya watakaofurahia huduma ambazo za kifedha zinazotolewa na benki hiyo ambayo kwa sehemu kubwa imejikita kutoa huduma kiteknolojia zaidi. Blog ya Jamii
No comments