Header Ads

ad

Breaking News

TPB Benki yaipaisha Taswa SC



Ofisa Mawasiliano wa Benki ya TPB, Chichi Banda (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi mwenyekiti wa Timu ya Waandishi wa mchezo nchini (Taswa SC) Majuto Omary ikiwa sehemu ya udhamini wao kwa timu hiyo kwa ajili ya kushiriki katika bonanza la waandishi wa habari wa Kanda ya Kaskazini.
Mwenyekiti wa Timu ya Waandishi wa mchezo nchini (Taswa SC) Majuto Omary (kushoto) akizungumza katika hafla ya kupokea mfano wa hundi kutoka Benki ya TPB.  kulia ni Afisa Mawasiliano wa Benki ya TPB, Chichi Banda.
Ofisa Mawasiliano wa Benki ya TPB, Chichi (kulia) Banda akizungumza jambo mara baada ya kukabidhi mfano wa hundi kwa Mwenyekiti wa Timu ya Waandishi wa mchezo nchini (Taswa SC) Majuto Omary

 
Mwandishi Wetu

Benki ya TPB imesaidia timu ya Soka na netiboli ya waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa Sc) iliyoondoka Jumamosi jijini Dar es Salaam kwenda Arusha kushiriki bonanza la vyombo vya Habari.

Ofisa Mawasiliano wa TPB Benki, Chichi Banda amesema kuwa wameisaidia Taswa SC kutokana na kutambua mchango wao katika kuendeleza michezo kwa vitendo huku wakiwa ni waandishi wa habari.

Chichi amesema kuwa wamevutiwa sana Taswa SC ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano mbalimbalimbali ikiwa pamoja na kuwa mabingwa wa kihistoria ya bonanza la vyombo vya habari la kanda ya Kaskazini.

“Hii ni faraja kwetu na tunaomba Taswa SC kuendeleza wimbi la ushindi katika bonanza hilo, tunaomba muendelee kufanya vyema ili kujiwekea historia zaidi,” amesema Chichi.

Mwenyekiti wa Taswa SC, Majuto Omary aliipongeza TPB Benki kwa msaada huo na kuomba wadau wengine kuunga mkono juhudi za benki hiyo kongwe nchini kuwasaidia waandishi wa habari.

"Kuna wadau wengi sana wa waandishi wa habari, tumepeleka maombi kwao, wengine wametujibu kwa simu tena siku mbili kabla ya kuanza safari kuwa hawana bajeti na wengine wamekaa kimya kabisa, imetusikitisha sana, tunawashukuru TPB Benki ambao wamekuwa na sisi kila tunapowahitaji,” amesema Majuto.

Majuto amesema kuwa waandishi wa habari ni wadau wakubwa katika sekta ya michezo na wamekuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya sekta hiyo, lakini mara kadhaa wamekuwa wakikumbana na vikwazo vikubwa katika shughuli ambazo zinawahusisha wao moja kwa moja.

“TPB Benki ni wadau wakubwa sana kwa Taswa SC, tunawapongeza kwa kujitolea kufanikisha shughuli hii ambayo sasa kila mchezaji (Mwandishi) ana uhakika wa kusafiri na kwenda kutetea ubingwa huku Arusha,” alisema Majuto.

Taswa SC imerejea jijini Dar es Salaam Jumatatu ikiwa na imetwaa ubingwa wa soka, netiboli na kukimbiza kuku.

No comments