MIKOA YETU TZA: Mtoto wa jinsia mbili kitendawili amtoa mama machozi
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgBtoTSH0zYwDx0KkIubGEhCDwljqMdGMW_Fr1khrTuermbUi-SMtY_1qNLyTPkZMvSC289kprStbHV5xaFUiWuBp8sASZZ6Vu1iqNcqWAdkSnXvpwHpKrSlFfy_IGNBE7vf67D1ahQ2M75/s640/unnamed+%25288%2529.jpg)
MSICHANA
wa miaka 19, Elizabeth Chengula anaelezea anavyoishi maisha ya shida
ambayo ni pamoja na kupata mtoto mwenye tatizo la utata wa jinsi yake
huku madaktari wakifafanua tatizo hilo kitaalamu.
Akizungumza
na gazeti hili hivi karibuni, Chengula alisema Agosti mwaka jana
alijifungua mtoto ambaye aliambiwa katika Zahanati ya Ifisi iliyoko
Mbalizi Mbeya Vijijini kuwa mtoto huyo ni wa kiume, lakini siku
zinavyozidi kwenda hajui ni wa jinsi gani baada ya maumbile yake ya siri
kuwa hayaeleweki ni ya kike au ya kiume.
Chengula alisema alipompeleka
hospitali huko Mbeya aliambiwa kuwa tatizo hilo ni mpaka ampeleke
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini kutokana na hali yake ya
maisha kuwa duni, hakuwa na uwezo wa kufika Dar es Salaam iliko
hospitali hiyo.
“Hali
hii ilinichanganya sana nikaenda kuomba msaada Ofisi ya Mkuu wa Wilaya,
walinisaidia nikachangiwa pesa kwenye ofisi yao ikapatikana laki mbili
na orobaini, nikapewa kwa ajili ya safari pamoja na barua ya rufaa, hata
hivyo pesa hizo ziliibiwa zote pamoja na begi langu nikiwa safarini
kuja Dar es Salaam,” alieleza msichana huyo.
Akielezea maisha yake,
alisema mama yake ni mlemavu wa mikono na miguu ambaye hawezi
kujishughulisha na kitu chochote na yeye na mama yake wanaishi kwa ndugu
yao ambaye anafanya vibarua vya kubeba mizigo ya watu sokoni Mbalizi.
“Maisha
yangu ni ya shida sijui nitapataje msaada wa mtoto huyu ambaye
nimeambiwa Muhimbili anatakiwa kufanyiwa vipimo na baadaye kufanyiwa
upasuaji na mimi sina mtu yeyote wa kunisaidia,” alisema Chengula kwa
masikitiko.
Aliongeza kuwa pamoja na kwamba hana uwezo wa kumsaidia
mtoto wake, lakini anaamini atapata msaada mtoto wake aweze kuwa kama
watoto wengine ingawa baba wa mtoto huyo alimkimbia baada ya kuambiwa
mtoto ana tatizo.
“Baba
wa mtoto alisema hamtaki mtoto na nisimpe jina lake mtoto huyu ni mkosi
hataki kujihusisha naye, nahangaika peke yangu nikipata watu wa
kunisaidia nitashukuru kwa sababu mimi naamini sio mkosi na atapona,”
alieleza msichana huyo.
Aidha, alisema katika kipindi chote hicho
amemlea mtoto wake kama wa kiume na alimpa jina la kiume ingawa hajui
jinsi yake.
“Kipindi
chote hicho mimi namlea kama mtoto wa kiume kwa mavazi na jina nimempa
la kiume, sasa nikiambiwa ni wa kike sijui nitaenda kuwaambia nini watu
kule nyumbani, nadhani nitahama kabisa na sijui nitaenda wapi maana
hawatanielewa,” alibainisha.
Watoto kuzaliwa na jinsi mbili au
isiyoeleweka Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Watoto, Zaituni Dkhary
akizungumzia tatizo hilo, alisema mzazi yeyote anaweza kupata mtoto wa
namna hii na kwamba tatizo hilo sio mkosi.
Dk
Dkhary alisema wazazi mwanzoni huwa wanachanganyikiwa kwa sababu
hawajui kama wataweza kuwa kawaida yaani wa jinsi moja walivyo watu
wengine au la, lakini tatizo hilo lina ufumbuzi.
“Na hakuna kesi yoyote
ambayo tumeipata mzazi kurudi kulalamika kwamba kuna hali tofauti
imetokea baada ya kuwasaidia, hapa Muhimbili tunawafanyia upasuaji
vizuri kabisa kuwarekebishia maumbile na wanakuwa sawa kabisa,” alieleza
Dk Dkhary.
Alisema
madaktari wanaofanya upasuaji huo ni madaktari bingwa wa upasuaji wa
watoto (Pediatric Surgeon) au madaktari bingwa wa upasuaj wa njia ya
mkojo (Urologist Surgeon) na kama kuna kesi ngumu wanaweza kusaidiana
lakini upasuaji huo ni wa kawaida kabisa.
Daktari huyo alisema watoto
ambao wanazaliwa wakiwa na maumbile hayo ni vigumu kuelewa jinsia yake
kwa kumtazama kwa macho katika sehemu zake za siri kwani wanakuwa na
viungo vya jinsia ya kike na pia ya kiume.
“Watoto
hawa kwa mzazi hata mzalishaji inakuwa ni vigumu kutambua kwa kuangalia
kwa sababu ukimuangalia mtoto sehemu zake za siri anakuwa na kiungo cha
kiume na pia maumbile ya kike na kwa chini anakuwa na tundu la
kukojolea,” alieleza.
Anasema katika hospitali hiyo wanapokea watoto
waliozaliwa katika hali hiyo wengi ambapo karibu kila wiki wanawafanyia
upasuaji wa kurekebisha maumbile baada ya kuwafanyia vipimo mbalimbali
na kubaini jinsi yake.
“Kama
ni mtoto wa kike utamfanya awe wa kike kwa kurekebisha maumbile yake,
na kama ni wa kiume hivyo hivyo, na ni lazima kufanya vipimo kadhaa
kwanza ili kuhakikisha jinsi ya mtoto,” alisema na kuongeza kuwa hakuna
sababu maalumu inayoweza kusababisha kupata mtoto mwenye tatizo hilo.
Alitaja
vipimo hivyo kuwa ni pamoja na vya damu kujua vinasaba vya mtoto na pia
kuchukua kijinyama kwenye mdomo wa mtoto kupima baada ya kuiotesha
pamoja na kipimo cha MRI kuona viungo vya ndani vya mtoto ni vya jinsi
gani.
CHANZO HABARI LEO
No comments