Balozi Kairuki ataka Watanzania kuchangamkia soko la muhogo nchini China
![]() |
Rais John Magufuli akimuapisha Mbelwa Kairuki kuwa Balozi wa Tanzania nchini
China, Ikulu jijini Dar es salaam Januari 20, 2017. |
Idara ya Habari (MAELEZO)
Balozi wa Tanzania nchini China,
Mbelwa Kairuki, amewataka Watanzania kujikita katika kilimo cha muhogo
baada ya zao hilo kupata soko la uhakika nchini China.
Balozi Kairuki alielezea fursa
hiyo ya soko mwishoni mwa wiki alipofanya mahojiano na Idara ya Habari
(MAELEZO) kuhusiana na fursa za biashara zinazopatikana China ambazo
Tanzania inaweza kuzitumia ili kukuza uchumi.
Alieleza kuwa mwezi Mei mwaka
huu, Serikali kupitia Ubalozi wake nchi China walisaini mkataba ambao
unairuhusu Tanzania kuuza zao muhogo katika nchi hiyo, fursa ambayo
Watanzania wanapaswa kuitumia kikamilifu kwa kufanya kilimo cha kisasa
ili kuzalisha kwa wingi zao hilo kwa ajili ya kuuza nje.
“Tukichangamkia hii fursa ya
muhogo tunaweza kusafirisha tani nyingi. Tunaweza hata kuanza kwa
kusafirisha muhogo wenye thamani ya dola milioni 500 na baadae tukikua
tunaweza kusafirisha muhogo wenye thamani ya bilioni mbili hadi tatu kwa
mwaka”, alieleza Balozi Kairuki.
Alieleza kuwa kwa sasa Nigeria
ndiyo nchi pekee kutoka Afrika ambayo inauza muhogo nchini China na
inakusudia kuuza tani milioni 150 za muhogo na kwamba kijiografia
Tanzania ina nafasi nzuri zaidi ya kuuza zao hilo kuliko Nigeria ambayo
ni ya nne duniani kwa kuuza muhogo nchini China, ikitanguliwa na
Thailand, Brazil na Indonesia.
Ili kulima kilimo chenya tija,
Balozi Kairuki alishauri Watanzania kutumia teknolojia ya kisasa katika
kuzalisha muhogo ikiwemo ile inayotumiwa na nchi ya Thailand ambayo
hekta moja inazalisha mpaka tani 25 au teknolojia ya China ambayo hekta
moja inazalisha tani 15 hadi 20 tofauti na Tanzania ambapo hekta moja
huzalisha tatu hadi saba.
Alieleza kuwa ili kutatua
changamoto katika kilimo cha muhogo, ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana
na mamlaka za China na Watanzania wanaosoma China katika fani ya kilimo
wamejaribu kuzishawishi taasisi za utafiti za China zishirikiane na
taasisi za Tanzania ili kuwezesha kupata mbinu za kuongeza uzalishaji.
Aidha, Balozi Kairuki ametoa wito
kwa wadau wote wa kilimo ikiwemo Wizara ya Kilimo, halmashauri pamoja
na Kituo cha Utafiti cha Naliendele kuunganisha nguvu pamoja ili kutatua
changamoto katika zao la muhogo na kuwawezesha wakulima kutumia vizuri
fursa ya soko la muhogo nchini China.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania
ni nchi ya nne kwa uzalishaji muhogo barani Afrika ikitanguliwa na nchi
za Nigeria, Ghana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
No comments