UWEKEZAJI WAONGEZEKA KATIKA SEKTA YA UTALII- MAKANI
Daudi Manongi-MAELEZO, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya
Maliasili na Utalii imesema kumekuwa na ongezeka la uwekezaji katika
miundombinu na mahitaji yanayochangia ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Ramo Makani wakati
akijibu Hoja mbalimbali za Wabunge .
“Kumekuwa na Ongezeko la uwekezaji
katika ujenzi wa Hoteli na Madaraja mbalimbali,uimarishaji wa vyombo
vya usafiri kuelekea ndani ya Hifadhi na Maeneo mengine yenye vivutio na
uboreshaji wa vifaa mbalimbali vinavyotumika kuhudumia watalii,mambo
ambayo kwa kiwango kikubwa hutekelezwa na Sekta binafsi “Aliongeza
Mhe.Makani.
Aidha amesema mafanikio hayo
yamewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii ambapo mwaka 2016 idadi hiyo
iliongezeka kutoka jumla ya Watalii milioni 1,137,182 kwa mwaka 2015
hadi jumla ya watalii 1,284,279 kwa mwaka 2016 sawa na ongezeko la
asilimia 12.9 ambapo ongezeko hilo limeonekana katika Hifadhi za Taifa
zinazosimamiwa na Tanapa.
Ameongeza kuwa ili ongezeko ili
liwe na tija na endelevu Wizara hiyo imejikita katika kusimamia ubora wa
huduma na utoaji huduma,kutangaza zaidi vivutio hususani vivutio vipya
na kusambaza shughuli za Utalii nchi nzima hususani ukanda wa kusini.
“Kwa upande wa Serikali ujenzi wa
barabara na viwanja vya Ndege,Ununuzi wa ndege mbili na zingine nne
zinatarajiwa kuja katika siku za karibuni izi zote ni jitihada
zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Utalii nchini”Alisisitiza
Mhe.Makani.
Pamoja na hayo ametoa wito kwa
Sekta Binafsi kuongeza mbinu,bidii na mitaji kuunga mkono jitihada za
Serikali katika kukuza Utalii na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.
No comments