Rais Muhammadu Buhari arejea London kwa matibabu
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amerejea London kupokea matibabu wiki chache baada yake kukaa huko kwa miezi miwili.
Taarifa kutoka kwa ikulu ya rais huyo imesema amehitajika kwenda Uingereza kuchunguzwa na madaktari.
Hata hivyo, kufikia sasa hakuna taarifa kuhusu ugonjwa anaougua wala muda ambao anatarajiwa kukaa nchini Uingereza.
Mwandishi
wa BBC Tomi Oladipo anasema Jumapili ilikuwa siku muhimu kwa Muhammadu
Buhari ambapo alikuwa anakutana na wasichana 82 wa Chibok ambao walikuwa
wameachiwa huru baada ya kuzuiliwa na wanamgambo wa Boko Haram kwa
miaka mitatu.
Badala yake, kutokana na afya yake, tukio hilo la kuwapokea halikufanywa kuwa sherehe kubwa.
Buhari amekuwa haonekani sana hadharani kipindi kirefu cha mwaka huu.
Alikaa wiki saba Uingereza kabla ya kurejea Machi.
Wiki iliyopita, hakuhudhuria mikutano mitatu ya baraza la mawaziri huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu hali yake.
Alijitokeza hata hivyo Ijumaa wakati wa swala ya Ijumaa katika msikiti ulio ikulu ya nchi hiyo.
Taarifa
kutoka ikulu imesema kiongozi huyo alikuwa amepangiwa kuondoka mapema
Jumapili alasiri lakini akachelewa kwa muda kumuwezesha kukutana na
wasichana hao wa Chibok.
Rais Buhari amesema: "Nina imani kwamba serikali itaendelea kutekeleza shughuli zake vyema nitakapokuwa nje ya nchi." (BBC)
No comments