Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete Afanya Ziara Tripoli, Libya
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais wa Baraza la Taifa (High State Council) wa Libya Mhe. Abdulrahman Asswehly jijini Tripoli, Libya. |
Rais
Mstaafu na Mjumbe Maalum wa AU katika Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya
jana tarehe 10 Mei amefanya ziara jijini Tripoli, Libya kuzungumza na
wadau muhimu wa siasa wa Libya. Safari hiyo ni ya kwanza kuifanya nchini
Libya tokea kuteuliwa kwake kuwa Msuluhishi wa mgogoro huo.
Akiwa
jijini Tripoli, Rais Mstaafu na ujumbe wake kutoka Kamisheni ya Umoja wa
Afrika amekutana na Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la
Libya Mhe. Fayez Serraj na Rais wa Baraza Kuu la Libya (High State
Council) Mhe Abdulrahman Asswehly.
Katika
mazungumzo yake na viongozi hao, Rais Mstaafu amewapongeza kwa hatua
madhubuti walizochukua katika kuimarisha hali ya usalama jijini Tripoli
ambapo theluthi moja ya wakazi wa Libya huishi humo. Amejionea na
kufurahishwa kwa kurejea na hali ya usalama na shughuli za kijamii na
kiuchumi.
Ameelezea
dhamira ya Umoja wa Afrika kuendelea kusaidia pande zinazotofautiana
ndani ya Libya kufikia makubaliano. Amesisitiza kuwa suluhisho la
mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe. Ameunga
mkono dhamira njema ya pande zinazotofautiana kupitia upya baadhi ya
vipengele vya Mkataba wa Makubaliano wa Siasa (Libya Political
Agreement) kwa lengo la kuuimarisha.
Kwa
upande wao, viongozi hao kwa nyakati tofauti wamemshukuru Rais Mstaafu
kwa kufanya ziara Libya na wamepongeza kwa uamuzi wake huo.
Wameichukulia ziara hiyo kuwa ni imani kubwa juu ya kuimarika kwa hali
ya usalama nchini mwao. Wameelezea dhamira yao ya kuendeleza Mkataba wa
Makubaliano uliopo na kutumia njia ya mazungumzo kumaliza tofauti
zilizopo. Wameomba Umoja wa Afrika kuendelea kusaidia jitihada za amani
na kuchangia uzoefu katika kusuluhisha mgogoro wao.
Rais Mstaafu anaendelea na ziara yake nchini Libya kwa kukutana na viongozi wa upande wa Mashariki mwa Libya.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri Mkuu na
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Libya Mhe. Fayaz Serraj jijini
Tripoli, Libya
No comments