NEC yaanza kutekeleza mpango wa elimu ya mpiga kura kupitia redio
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa elimu ya mpiga kura
kupitia redio A FM ya mkoani Dodoma leo Mei 9 mwaka huu huku
akifuatiliwa kwa makini na watangazaji wa redio hiyo.
……………………….
Hussein Makame, NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini,
kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia redio za
kijamii kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akizungumzia
mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima ulioanza kutekelezwa Mei 8
mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango huo
wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini,
watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa masuala yote
muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.
“Tumepanga mpango, Tume itasambaa
nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpiga kura kwenye redio za kijamii
zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
alisema Bw. Kailima.
Alisisitiza kwa kutoa wito kwa
wananchi walioko maeneo ambayo Tume itakwenda kutoa elimu ya mpiga kura,
wasikilize na kuuliza maswali ili waweze kuelewa.
“Hii ni fursa kwa wananchi ambayo
muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo nawaomba wafuatilie ili waweze
kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya kura yatakuwa yamekwisha na
tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo tumeifanya.” Alifafanua
Bw. Kailima.
Utekelezaji wa mpango huo
umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa
elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro,
Morogoro, Mbeya na Dodoma.
Mikoa mingine itakayojumuishwa
kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo elimu hiyo
itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei hadi tarehe 20 Mei mwaka 2017.
Kundi la pili linatarajiwa kutoa
elimu hiyo kuanzia tarehe 24 Mei hadi tarehe 7 Juni mwaka huu katika
mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga, Lindi, Arusha, Tabora,
Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe na Simiyu.
Bw. Kailima alisema kuwa utoaji wa
elimu hiyo utajikita kwenye mada kuu ya Elimu ya Mpiga Kura
iliyogawanywa kwenye vipindi vitano, itakaytoolewa kwenye redio hizo
kulingana mada husika na wananchi kuuliza maswali na kujibiwa na
wawasilishaji wa mada hizo kutoka Tume.
“Ni mada ambayo imejumuisha
masuala yote muhumu yatakayofanya mpiga kura yeyote au mdau yeyote wa
uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa mfumo mzima wa masuala ya
kupiga kura” alisema.
Mbali na kutoa elimu ya mpiga kura
kupitia vituo vya redio za kijamii katika halmashauri nchi nzima, Tume
pia inatoa elimu hiyo kwa njia ya magazeti na vyombo vingine vya habari
na mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye mikutano na maonesho
mbalimbali nchini.
No comments