Header Ads

ad

Breaking News

Mourinho: Nafurahi mashabiki wa Arsenal walifurahi

Kocha wa Man United, Jose Mourinho
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema ana furaha kwamba mashabiki wa Arsenal hatimaye walipata jambo la kusherehekea baada ya kufanikiwa kulaza United 2-0 Jumapili.
Ushindi huo wa Arsenal ulikuwa wa kwanza wa Arsene Wenger katika mechi 16 za ushindani dhidi ya timu iliyokuwa chini ya Mourinho.
"Niliondoka Highbury na walikuwa wanalia, nikaondoka Emirates na walikuwa wanalia," Mourinho alisema kuhusu mechi za awali alizowahi kucheza na timu dhidi ya Arsenal kwao nyumbani.
"Hatimaye leo wanaweza kuimba, wanarusha skafu hewani. Ni jambo zuri kwao."
Aliongeza: "Ni mara ya kwanza kwamba naondoka na wamefurahi. Awali, walikuwa wakiondoka wanatembea wameinamisha vichwa barabarani.
"Mashabiki wa Arsenal wana furaha na nina furaha kwa sababu ya hilo."

Mechi pekee ambayo Arsenal waliwahi kushinda dhidi ya Mourinho wakiwa na Wenger ilikuwa mwaka 2015 wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii Mourinho alipokuwa Chelsea.
Klabu za wawili hao zilikutana mara ya kwanza Desemba 2004 - Gunners walipokuwa bado wanatumia uwanja wa Highbury - mechi iliyoisha kwa sare ya 2-2.
"Kuwa na rekodi kama hiyo ya kushinda mechi nyingi hivyo si jambo la kawaida. Kawaida ni unashinda, unashindwa, unatoka sare," Mourinho alisema.
"Mnafikiri huwa nafurahia hali kwamba klabu kubwa hivi kama Arsenal haishindi vikombe? Sifurahii kamwe. Hiyo ni klabu kubwa.
"Wenger si meneja mdogo. Yeye ni meneja mkubwa. Kwa hivyo si kawaida na sijali sana kuhusu hilo."

Baada ya kushindwa Jumapili, United sasa wamo alama nne nyuma ya wapinzani wao Manchester City walio nafasi ya nne.
Mourinho hata hivyo anaonekana kuangazia zaidi Europa League ambapo mshindi hufuzu moja kwa moja kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Watakutana na Celta Vigo mechi ya marudiano nusufainali Old Trafford Alhamisi, ambapo tayari wanaongoza 1-0 kutoka kwa mechi ya kwanza.

"Tunataka kujaribu kushinda Europa League - ni muhimu kuliko kumaliza nafasi ya nne. Nafikiri ni vigumu sana, ni kama karibu haiwezekani kufuzu kupitia (kumaliza katika nne bora) Ligi ya Premia," Mourinho alisema.
"Vikombe ndivyo huandika historia. Si kumaliza nafasi nzuri ligini. Tutajitolea kwa hali na mali hadi fainali.
"Mechi ya Alhamisi sio mechi muhimu zaidi msimu huu. Natumai Old Trafford itakuwa vile vile, kwa sababu tunaihitaji ikiwa vile vile Old Trafford." (BBC)

No comments