AZAM FC KUANDAA LIGI YA VIJANA KUANZIA U-11 HADI U-17
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, inayofuraha kutangaza uzinduzi wa programu ya Ligi za
Vijana za Azam (AYL), ambayo utaifanya klabu kuendesha ligi za vijana za
timu chini ya umri wa miaka 11, 13, 15 na 17 ndani ya mkoa wa Dar es
Salaam.
Kwa kuanzia, Azam FC itaanza na
Ligi ya Vijana ya chini ya umri wa miaka 13 itakayoanza Mei 27, mwaka
huu katika Uwanja wa Azam Complex, ambapo mechi zitakuwa zikifanyika
kila Jumamosi kwa muda wa wiki 10.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz
Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana la Azam FC, Tom Legg, alisema kuwa
wanayofuraha kufanya kazi na timu sita za hapa kwa kuanzia kwenye ligi
hiyo, ambazo ni Bom Bom SC, JMK Park Academy, Rendis FC, Ilala Academy,
Magnet Youth pamoja na wenyeji Azam, ambao wataumana kuwania taji la
michuano hiyo (U-13).
Legg alisema kuwa kutokana na
klabu kuonyesha dhamira ya uaminifu na uwazi katika maendeleo ya soka la
vijana, kila mchezaji atakayeshiriki michuano ya Ligi ya Vijana ya Azam
atatakiwa kutoa ushahidi wa utambulisho kuhusu umri wakati atakapokuwa
akijiandikisha kushiriki ligi hiyo.
“Taarifa hizo zitahifadhiwa kwenye
mtandao, zitashirikishwa miongoni mwa timu shiriki na zitakuwa
zikipatikana kwa makocha wote kwenye simu zao za kisasa ili kuhakikisha
kuwa kila mchezaji atakayecheza kwenye ligi hiyo atakuwa amesajiliwa na
Kamati ya Maandalizi na kuwa na umri sahihi,” alisema.
Mtaalamu huyo wa soka la vijana,
alisema kuwa hatua ya pili ya Ligi ya Vijana ya Azam, itakuwa ni
uzinduzi zile za chini ya umri wa miaka 15 na 17 utakaofanyika Agosti
mwaka huu, huku akidai katika siku chache zinazokuja Azam FC itatoa
taarifa za ziada kuhusu hili na kwa timu ambazo zitavutiwa kushiriki
kudhibitisha ushiriki wao kwa kujisajili.
Aidha alisema mipango ya hapo
baadaye ni kuendesha ligi za aina hiyo kwenye mikoa mingine ya Tanzania
na akiwa kama Mkuu wa soka hilo la vijana amedai kuwa amekuwa akifanya
kazi bila kuchoka uwanjani itakayopelekea hapo baadaye klabu kuipanua
zaidi programu hiyo.
Alisema lengo kuu la kuanzishwa
kwa programu ya Ligi ya Vijana ya Azam FC ni kuhakikisha klabu hiyo
inacheza nafasi kubwa katika maendeleo ya kutengeneza kizazi kijacho cha
wachezaji wa Tanzania.
“Tumekuwa na furaha tele hivi
karibuni kushuhudia mafanikio ya timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania
U-17 (Serengeti Boys) na tunawatakia mafanikio mazuri katika michuano
inayokuja ya Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) nchini Gabon…Kwa programu
hii tunaamini tutakuwa tumecheza sehemu muhimu katika harakati pana za
kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutoa timu katika michuano hapa
Afrika na Kimataifa kwa miaka mingi ijayo,” alimalizia Legg.
Hii ni michuano ya pili kwa Azam
FC kuandaa kwa upande wa vijana, ambapo mwaka jana iliandaa ile ya chini
ya miaka 20 kwa nchi za Afrika Mashariki na kushirikisha timu nne,
mbili kutoka Tanzania (Azam FC na Future Stars Academy – Arusha) na Ligi
Ndogo Academy (Kenya) na Football For Good Academy (Uganda), huku Azam
FC ikiibuka mabingwa.
No comments