WIZARA YAKEMEA UBAKAJI WA MTOTO MKOANI IRINGA
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakemea vikali tukio la kubakwa kwa binti wa miaka saba
(jina limehifadhiwa) mkazi wa kata ay Kitanzini, mwanafuzi wa darasa la
awali shule ya SUN Academy iliyoko kata ya Kwakilosa, manispaa ya
Iringa.
Wizara imesikitishwa na
taarifa za awali kuwa mtoto alibakwa katika mazingira ya shule mahali
ambapo tunategemea pawe salama kwa mtoto kuishi. Wakati wote Serikali
imekuwa ikisisitiza walezi wa watoto kuhakikisha wanalinda watoto dhidi
ya vitendo vyote vya ubakaji kwani vitendo hivi vimekuwa vikitaarifiwa
kuwahusisha watu wa karibu wanaomzunguka mtoto katika familia, shuleni
na jamii.
Wizara inapongeza vyombo vya
habari vyote vinavyoibua matukio ya ukatili, kwa kufanya hivyo ni sehemu
ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya
wanawake na watoto ambao utekelezaji wake unahusisha wadau wote nchini.
Wizara inamini kuwa Polisi kwa
kutumia weledi na umahiri wao watashirikiana na wananchi, walezi,
walimu na marafiki wa mtoto, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanafichuliwa
na kuchukuliwa hatua stahiki.
Wizara inawakumbusha wazazi na
walezi kuwa vitendo vya ukatili ukiwemo ubakaji dhidi ya watoto wa kike
havikubaliki katika nchi yetu kwani vitendo hivyo vinatia doa kubwa
taifa letu. Natoa rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika
kuwafichua waliohusika na ubakaji wa mtoto aliyeripotiwa kwa kutoa
taarifa kwenye mamlaka husika, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua
stahiki.
Erasto T. Ching’oro
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
No comments