WANAWAKE JIKITENI KATIKA UJASIRIAMALI, UTAWAKOMBOA
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Dunia ya sasa inapigania haki sawa
kwa wanaume na wanawake ili waweze kushiriki kwa pamoja kwenye nyanja
zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuchangia kwenye
ukuzaji wa pato la taifa na kupelekea kukua haraka kwa maendeleo ya
nchi.
Tumeshuhudia wanawake wengi nchini
wakijikita katika kufanya biashara na ujasiriamali wa bidhaa na huduma
mbalimbali ambazo zinawakomboa kiuchumi na kuwafanya waweze kujitegemea
kama walivyo wananume.
Wanawake hao waliojiamini na
kuamua kuanzisha biashara zao wameonekana kuwa na mafanikio makubwa
ambayo yanasaidia kuinua uchumi wa mtu binafsi na wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, baadhi ya
wanawake wamekua bado hawana ujasiri wa kuanza kufanya ujasiriamali kwa
kuhofia kuwa hawataweza kuendelea na wengine wakihofia waume zao
kuwakataza.
Dhima ya kujirudisha nyuma
waliyonayo baadhi ya wanawake ndio inayorudisha nyuma hata maendeleo ya
nchi hasa kwa wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeamua
kujikita katika kukuza uchumi wa viwanda.
Serikali inafanya jitihada
mbalimbali za kuwahamasisha wanawake kufanya ujasiriamali hivyo kupitia
Benki ya Wanawake, Serikali imeendelea kutoa huduma za mikopo kwa
wajasiriamali wanawake nchini ili kuhakikisha wanapata mitaji ya
kuanzishia shughuli hizo ambazo baadae zinakua ni mkombozi wa maisha
yao.
Katika kipindi cha 2009 hadi
2014, Benki ya Wanawake imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi
bilioni 24.9 kwa wananchi 12,992 wakiwemo wanawake 11,350 ambayo ni
sawa na asilimia 87.
Aidha, katika kuwawezesha
wanawake kiuchumi na kuinua hali zao kimaisha, Mfuko wa Maendeleo ya
Wanawake umenufaisha vikundi 3,119 vyenye jumla ya wanawake 23,769.
Idadi ya wanawake waliopata
mikopo kutoka katika Mfuko huo imeongezeka kutoka wanawake 3,008 mwaka
2005 hadi kufikia wanawake 23,769 mwaka 2014.
Pia jumla ya Mikoa 25 ya
Tanzania Bara ilipelekewa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa
ajili ya kuwakopesha wanawake, mikopo hiyo imewawezesha wajasiriamali
wanawake kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na hivyo
kuinua kipato chao.
Kwa upande wake Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema
kuwa jamii inatakiwa kuondokana na dhana ya mfumo dume inayomfanya
mwanamke kukaa bila kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi hivyo kuwa
mtegemezi kwa kila kitu hali inayopelekea kushindwa kutoa maamuzi
wanayoyataka na wengine kunyanyaswa.
Hivyo, jamii inatakiwa
kuhakikisha inashirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali
kuwajengea uwezo wanawake, kuwapa elimu na kuwapa fursa wanawake
kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali zikiwemo za kilimo na
biashara mbalimbali.
Ukiondoa mchango wa Serikali
katika kuwasaidia wanawake kujikwamua, wanawake wenyewe kwa wenyewe
wanatakiwa kusaidiana hasa wale walioendelea wanatakiwa kutoa elimu na
ushauri kwa wanawake wenzao ili kila mwanamke afahamu juu ya umuhimu wa
ujasiriamali na jinsi utakavyoweza kumkomboa katika maisha yake ya kila
siku.
Pia wanashauriwa kujiunga katika
vikundi vya kusaidiana ili kupeana mawazo mbalimbali ya biashara,
kutiana moyo kwa kuwa siku zote mwanzo wa kitu chochote huwa ni mgumu
pamoja na kusaidiana katika kupeana mitaji itakayowawezesha
wajasiriamali kuinuka.
Kufuatia maadhimisho ya Siku
ya wanawake Duniani,wanawake wa Tanzania wamepewa jukumu la kuhakikisha
wanajikita katika ujasiriamali na kushiriki katika kuinua uchumi kupitia
viwanda kwani wanawake ndio msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.
No comments