WANAODAIWA KUFANYA MAUAJI YA ALIYEKUWA DC WAKAMATWA PWANI
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MAKACHERO wa jeshi la polisi
mkoani Pwani,wakishirikiana na waliotoka makao makuu ya polisi
wanawashikilia watuhumiwa 16 akiwemo Khalid Mohammed (29)mkazi wa
Kwamatias,Kibaha ,wanaodaiwa kufanya uporaji na mauaji kwenye maeneo
mbalimbali.
Aidha baadhi ya watuhumiwa hao
wanadaiwa kuhusika katika tukio la mauaji ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya
Liwale tangu mwaka 2012 hadi 2016,Ephraim Mfingi Mbaga(54).
Akizungumzia tukio hilo,kamanda
wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi ,alieleza kwamba Khalid ambae
ni fundi ujenzi,alikamatwa juzi huko eneo la Misugusugu kata ya
Misugusugu.
Alisema mbali ya hayo ,alikamatwa akiwa na silaha aina ya SMG ambayo namba zake zimefutwa na risasi 14.
Kamanda huyo ,alisema alikutwa
pia na risasi nne za shortgun,mlipuko mmoja,sime moja,mask moja na koti
moja vyote vikiwa vimehifadhiwa kwenye mfuko wa rambo chini ya ardhi
katika shamba la aliyejulikana kwa jina moja la Swai.
Hata hivyo,kamanda Mushongi
alifafafanua kuwa,uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa na wenzake 15
wamekiri kujihusisha na matukio ya uporaji katika maeneo mbalimbali ya
mkoa huo.
“Tukio mojawapo ni mauaji ya
aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Liwale tangu mwaka 2012 hadi 2016, Ephraim
Mbaga,aliyeuawa akiwa nyumbani kwake baada ya kupigwa risasi kwenye
paja la mguu wa kushoto “
“Pia alijeruhiwa kwa kitu chenye
ncha kali ambapo alipoteza maisha akiwa njiani akipelekwa hospitali ya
rufaa ya Tumbi.”alisema.
Kwa mujibu wa kamanda
Mushongi,tukio hilo lililotokea februari 18 mwaka huu saa 3.30
usiku,ambapo watu watatu wanaosadikiwa ni majambazi walimpiga na kitu
kinachohisiwa ni silaha.
Alielezea ,marehemu alifariki njiani akipelekwa hospital ya rufaa ya Tumbi baada ya kuvuja damu nyingi.
Inaelezwa kuwa ,akiwa nyumbani kwake watu hao waliingia na kumtaka atoe pesa na aliposhindwa kufanya hivyo walianza kumjeruhi.
Katika eneo la tukio kilipatikana
kichwa cha risasi kinachodhaniwa kuwa ni 7.62 mm inayotumiwa na silaha
SMG/SAR ,na walifanikiwa kupora laptop mbili,simu za mkononi nne na vitu
vingine ambavyo bado havijafahamika.
No comments