WACHAPISHAJI NCHINI WAMETAKIWA KUJIANDIKISHA KWA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI
Jovina Bujulu- MAELEZO
Serikali imewataka wachapishaji
wote nchini waliojiandikisha kwa Msajili wa Makampuni ( BRELA) na
Mamlaka ya Mapato (TRA), kufika katika ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali ili wajiorodheshe na watambuliwe na Serikali na wananchi
kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Dar es
salaam na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ndugu Cassian Chibogoyo alipokuwa
akizungumzia kuwepo kwa wimbi kubwa la wachapishaji hewa nchini.
Chibogoyo amesema kuwa hatua hiyo
inafuatia uwepo wa utitiri wa wachapishaji ambao hawatambuliki na
Serikali, kwa sababu baada ya kujiandikisha kwa mamlaka husika kama
kampuni, utawakuta wana mitambo ya uchapishaji ambayo mara nyingi
wanaitumia kuchapisha nyaraka bandia za Serikali bila kuwa na kibali
kutoka katika mamlaka yenye dhamana ya uchapishaji.
“Kwa sasa tumeanzisha utaratibu
maalum wa kuwatambua wachapishaji ambapo wanatakiwa kujiorodhesha kwa
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, hii ni kutokana na kuwepo kwa uchapaji
holela na bandia wa nyaraka za Serikali” alisema Chibogoyo.
Aliongeza kuwa chini ya utaratibu
uliowekwa sasa wachapishaji wanatakiwa kuwasilisha nyaraka halali za
kampuni, shughuli wanazofanya, historia ya kampuni na mahali kampuni
inapofanyia kazi zake.
Adha, Chibogoyo alisema kuwa
faida za wachapishaji kujiandikisha ni pamoja na kutambuliwa kisheria na
Serikali ili hata wanaposhutumiwa waweze kulindwa na Serikali,
kukumbushana majukumu yao , wigo wao wa kazi, na pia wataelimishwa
kuhusu nyaraka wanazopashwa kuchapisha maana si kila nyaraka wanapashwa
kuzichapisha.
Zaidi ya hayo, Chibogoyo alitaja
madhara ya kuchapisha nyaraka bandia kuwa ni pamoja na kuikosesha
Serikali mapato kutokana na uchapishaji wa stakabadhi mbalimbali bandia,
uvamizi wa mawasiliano ya Serikali uchapishaji wa vyeti vya usajili wa
makampuni, na uchapishaji bandia wa vyeti vya elimu ambavyo hupelekea
mtu kuajiriwa kwa kazi ambayo hana ujuzi nayo.
Akizungumzia hatua ambao zinaweza
kuchukuliwa dhidi ya wachapishaji wa nyaraka bandia, Chibogoyo alisema
kuwa ni pamoja na kutaifisha mitambo ya wahusika.
Akizungumza suala hilo hivi
karibuni katika kipindi cha “Tujikumbushe”, Chibogoyo alisema kuwa
makosa ya uhalifu wa nyaraka bandia yanaangukia katika sheria za
ushahidi, sheria ya makosa ya jinai, sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka
1970, pamoja na sheria ya nembo na alama za Taifa.
Mpiga Chapa huyo Mkuu wa Serikali
alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kupambana na vita hii
kwa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ili kutokomeza janga
hilo.
“Tunawaomba wananchi tuwe na
mshikamano katika kufichua janga hili la uchapishaji holela na bandia
kwani ni janga la kitaifa, linagusa maslahi ya nchi na wananchi,
nalifananisha na ujambazi wa hali ya juu” alisisitiza Chibogoyo.
Baadhi ya nyaraka ambazo zimekuwa
zikighushiwa mara kwa mara ni pamoja na vyeti vya elimu katika ngazi
mbalimbali, risiti za serikali, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, kadi za
magari na pikipiki, mihuri na nembo ya Taifa.
No comments