TADB, BODI YA NYAMA KUWAWEZESHA WADAU WA UFUGAJI WA NG’OMBE
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (Kulia)
akiwakaribisha maafisa kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB)
walipomtembelea Ofisini kwake kujadiliana juu ya Mkutano Mkuu wa Wadau
wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9
Machi, 2017. Kushoto ni Afisa Masoko na Utafiti, Bw. Nicholai Chiweka na
Afisa Sheria, Bw. Praisegod Lukio (katikati).
Afisa Masoko na Utafiti wa TMB,
Bw. Nicholai Chiweka (aliyeinama) akisaini Kitabu cha Wageni wakati
alipomtembelea TADB. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga (kushoto), Afisa Sheria wa TMB, Bw. Praisegod Lukio
(wa pili kushoto). Kulia ni Mkuu wa Huduma na Sheria wa TADB, Bibi
Neema Christina John.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga (kushoto) akizungumza na maafisa kutoka Bodi ya
Nyama Tanzania (TMB) Afisa Sheria, Bw. Praisegod Lukio (wa pili kushoto)
na Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (wa pili kulia)
wakati walipomtembelea Ofisini kwake kujadiliana juu ya Mkutano Mkuu wa
Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8
hadi 9 Machi, 2017. Kulia ni Mkuu wa Huduma na Sheria wa TADB, Bibi
Neema Christina John.
Afisa Masoko na Utafiti wa TMB,
Bw. Nicholai Chiweka (kulia) akizungumza wakati walipomtembelea Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB (hayupo pichani) kujadiliana juu ya Mkutano
Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia
tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga (wa pili kushoto) na Afisa Masoko na Utafiti wa
TMB, Bw. Nicholai Chiweka (wa pili kulia) wakionesha fulana kwa ajili ya
Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma
kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017. Wengine pichani ni Mkuu wa Huduma
na Sheria wa TADB, Bibi Neema Christina John (kushoto) na Afisa Sheria
wa TMB, Bw. Praisegod Lukio (kulia).
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) na Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) zimejidhatiti kusaidia
mnyororo wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa ili
kuongeza tija kwenye sekta ya ufugaji wa ng’ombe nchini.
Hayo yamebainishwa na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga na Afisa Masoko na
Utafiti, Bw. Nicholai Chiweka kutoka TMB wakati wa majadiliano kuhusu
Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma
kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.
Bw. Assenga amesema kuwa TADB
imejidhatiti katika kuongeza tija kwa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na
Maziwa kwa kutoa mikopo na kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji
tija wa ufugaji huo.
“Katika kuhakikisha sekta hii
inaendelea na kuongeza tija, TADB imejipanga kutoa mikopo itakayotumika
kama mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa mashamba, uongezaji wa thamani na
gharama za uhifadhi wa nyama/maziwa na miundombinu masoko kwenye sekta
hii,” alisema Bw. Assenga.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB
ameongeza kuwa kwa kushirikisha wadau wa Kilimo, utafiti, huduma za
ugani na madaktari wa mifugo TADB imelenga kuwapatia wafugaji mafunzo ya
ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa kwa kutumia mbinu bora
za ufugaji ili kufuga kibiashara na hivyo kujiongezea kipato na
kupambana na umaskini.
Kwa upande wake Bw. Chiweka
amesema kuwa TMB ina Mamlaka yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya
tasnia ya nyama, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006
hivyo ina wajibu wa kuratibu mnyororo mzima wa thamani wa tasnia ya
nyama na kuiomba TADB kushirikiana na TMB kunyanyua sekta ya nyama.
“Kifungu Na. 17 (1) cha sheria
hii, kinazuia mtu yeyote kufanya shughuli ya aina yoyote katika tasnia
ya nyama bila ya kuwa na cheti cha usajili kutoka Bodi ya Nyama Tanzania
hivyo kama mdau wa kuendeleza sekta hii tunaiomba TADB kuwasaidia wadau
wa mnyororo mzima wa thamani wa tasnia ya nyama ambao wamesajiliwa na
TMB,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Chiweka wadau wa
tasnia ya nyama inajumuisha Wafugaji wa mifugo ya aina zote
inayozalisha nyama; Wafanyabiashara wa Mifugo; Wasafirishaji wa mifugo
na nyama; na Wenye machinjio za aina zote. Wengine ni Wenye bucha za
kuuza nyama za aina zote; Wasindikaji wa nyama; maduka makubwa na duka
la bucha, Wasambazaji wa bidhaa za nyama; Waingizaji wa nyama nchini;
Wasafirishaji wa mifugo, nyama na bidhaa zake nje ya nchi; na Waendesha
matamasha ya nyama choma.
Mnyororo wa thamani wa Ufugaji wa
ng’ombe wa nyama na maziwa ni miongoni mwa minyororo ya mwanzo
inayopatiwa mikopo na TADB ili kuongeza thamani mazao na mifugo
mbalimbali nchini.
No comments