Header Ads

ad

Breaking News

PEMBA: NAIBU WAZIRI AWATAKA WAFANYA KAZI KUACHA TABIA YA KUPIKIANA MAJUNGU NA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

SHATA
Na Masanja Mabula –Pemba  .
NAIBU Waziri wa Wizara ya Nchi , Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa , Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Shamata Shaame Khamis amewataka wafanya kazi wa Ofisi ya Baraza la Mji Wete kuacha tabia ya kupikiana majungu na  kufanya kazi kwa mazoea .
Akizungumza na wafanyakazi na Viongozi  wa Baraza la Mji Wete ,katika Ukumbi wa Jamhuri  amesema majungu ni sumu ya mafanikio ya kazi , hivyo ni vyema kujiepusha na tabia hiyo ili kuongeza ufanisi wa kazi zao za kila siku .
Amesema  bado watendaji wa Baraza hilo wamekosa ushirikiano  jambo ambalo linatia hofu kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya Baraza la Mji .
“Si vyema kuhusika na masuala ya kupikiana majungu sehemu za kazi , nawaomba mfanye kazi za kutekeleza wajibu wenu kwa mujibu wa taratibu na miongozi  wa utumishi ”alisisitiza.
Aidha ametaka uwepo na usimamizi mzuri na utumiaji wa fedha zinazokusanywa kwa kuhakikisha zimetumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayoibuliwa na wananchi pamoja na Serikali Kuu .
“Hakikisheni kuna ushirikiano wa kutosha miongoni mwenu , na hii itasaidia kuwepo na usumamizi mzuri wa fedha zinazokusanywa na kwamba zitatumika kwa ajili ya kazi za maendeleo ya jamii ” alisema.
Naibu Waziri amemwagiza mwanasheria wa Baraza hilo kuandaa utaratibu wa kuwaelimisha wanafanyakazi na watendaji wa baraza ,  kufuata taratibu na Sheria ili kuepuka uvujaji wa mapato .
Nao wafanyakazi wa baraza hilo wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo  uhaba wa wafanayakazi, jambo linalochangia mji huo kuwa katika hali isiyo ya kuridhisha.

No comments