JESHI LA MAGEREZA KUPOKEA MAGARI 450 AINA YA ASHOK LEYLAND
Lucas Mboje, Dar es Salaam
KAMISHNA Jenerali wa Magereza
nchini, Dkt. Juma Malewa(pichani) ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha mchakato wa
ununuzi wa magari 450 ya Jeshi hilo ambayo yanatarajiwa kupokelewa muda
wowote kuanzia sasa.
Kamishna Jenereli Malewa ameyasema
hayo leo katika ufunguzi rasmi wa mkutano wa wakuu wa magereza yote
Tanzania Bara unaofanyika kwa siku moja katika Bwalo kuu la Maafisa
magereza, ukonga jijini Dar es Salaam.
Jenerali Malewa amesema kuwa
upatikanaji wa magari hayo utapunguza tatizo kubwa la uhaba wa magari
kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na utawala pamoja uboreshaji wa
utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru
kwa dhati Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na serikali yote kwa
ujumla kwa namna inavyoshughulikia utafutaji wa ufumbuzi wa changamoto
tulizonazo,” alisema Jenerali Malewa.
Aidha kuhusu madeni ya Watumishi
wa Jeshi hilo na wazabuni, Kamishna Jenerali Malewa amesema serikali
imetoa kiasi cha zaidi ya Bilioni 8 za pesa ya kitanzania kwa ajili ya
kulipa madeni hayo ambapo madeni yote yaliyokwisha kuhakikiwa tayari
yameanza kulipwa na wahusika wamekwishaanza kupata fedha wanazodai Jeshi
hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuph Masauni akizunguza katika
ufunguzi wa Mkutano huo ametoa rai kwa jeshi hilo kutumia vyema fursa
zilizopo katika katika maeneo mbalimbali ya jeshi hilo kwa kuanzisha na
kuimarisha viwanda vidovidogo vilivyopo ili kuongeza uzalishaji hivyo
kuchangia pato la taifa.
Masauni amesema kuwa Jeshi la
Magereza linazo fursa nyingi sana za uzalishaji yakiwemo maeneo makubwa
yanayofaa kwa kilimo, miradi ya ufugaji na miradi mengineyo ya kiuchumi.
“Nisisitiza kwamba wekeni mikakati
yenye lengo la kuongeza uzalishaji katika maeneo yenu kwani nataka kila
mmoja wenu katika gereza alilopo aweke malengo ya kuongeza uzalishaji
kulingana na fursa zilizopo,” alisema Mhe. Masauni.
Mkutano huu wa Wakuu wa Magereza
yote Tanzania Bara unajumuisha Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya
Magereza na Wakuu wa vituo vya Magereza yote nchini ambapo lengo kuu ni
kujadiliana kwa kina hali halisi ya utendaji kazi magerezani na kuweka
mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuongeza tija na
ufanisi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni Jeshi la Magereza katika jitihada za kufanikisha kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda.
No comments